Wednesday, August 21, 2013

RAIS WA ZAMANI WA MISRI MUBARAK KUACHIWA HURU KWA DHAMANA.

Mahakama nchini Misri inatarajia kutoa uamuzi wa ama kumuachia huru kwa dhamana au la, Rais wa zamani nchi hiyo Hosni Mubarak.

Bwana Mubarak anakabiliwa na mashtaka ya rushwa ambayo yamemfanya asalie rumande bila dhamana.

Rais huyo wa zamani wa Misri mwenye umri wa miaka 85 pia anakabili kesi nyingine ya kushirikiana katika mauji ya waandamanaji wakati wa vuguvugu la mapinduzi ya kiraia yaliyomuondoa madarakani mwaka 2011.

Wakati huo huo, Mawaziri wa mambo ya nje na masuala ya kigeni wa nchi za umoja wa Ulaya wanakutana kujadili hatima ya Misri, huku wengine watarajia kufuta kabisa misaada yote kwa taifa hilo lililopo kwenye hali tata kwa sasa.

Baadhi ya mawaziri wameomba fungu la msaada wa Yuro bilioni 5 sawa na dola Bilioni 6.7 wanalopewa Misri kufutwa baada ya watu zaidi ya 900 kuuwawa kwenye ghasia tangu wiki iliyopita.

Vifo hivyo vimetokea mara baada ya serikali ya mpito kuamuru vikosi vya polisi na jeshi kufunga kambi mbili za wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi.

 

Bwana Mubarak 85,alishitakiwa mwezi Juni mwaka 2012 kwa mashtaka ya kuhusika na mauaji ya waandamanaji mwaka 2011 na kufungwa kifungo cha maisha jela.

Lakini mwezi Januari 2013 alishinda rufaa aliyokata na mahakama ya rufaa kuamuru kesi yake isikilizwe upya.

Kesi hiyo ilianza upya mwezi Mei 2013,lakini bwana Mubarak tayari amekwishakaa kizuizini kupita muda ambao unatakiwa kwa mashtaka hayo.

Wakili wa Mubarak , Fareed Al Dib amesema anatarajia mteja wake ataachiliwa huru baada ya amri ya mahakama na atasalia na kesi za mashitaka dhidi ya rushwa pekee.

Licha ya upande wa mashitaka kutarajiwa kupinga kwa kukata rufaa dhidi ya kuachiwa kwake,jambo ambalo litachelewesha kutoka kwake gerezani.

Kesi hiyo pia inahusiana na tuhuma za rais huyo kupokea hongo kama zawadi kutoka kwa gazeti la serikali Al-Ahram.

kuna habari kutoka katika familia ya Mubarak zinasema kuwa imelipa gharama zote na zawadi ambazo anadaiwa kuzichukua, suala ambalo linamuongezea matumaini wakili wake kuwa huenda mteja wake akaachiliwa huru.

Hukumu ya rufaa itasomwa kwenye gereza ambalo Mubaraq amefungwa.

Wadadisi wanasema iwapo Mubarak ataachiliwa, hiyo itarudisha hisia za wengi za kwamba jeshi linataka kurejesha utawala ambao uliondolewa kwa mapinduzi ya kiraia ya mwaka 2011,

Suala ambalo huenda likarudisha maandamano makubwa na ghasia zaidi kuendelea kuzuka nchini humo.


No comments:

Post a Comment