Mkongwe katika muziki Muhidin Maalim Gurumo mwenye miaka73 Pichani wa Bendi ya Msondo Ngoma,
ametangaza kustaafu fani hiyo baada ya kutumbuiza jukwaani kwa miaka 53.
Gurumo aliyeimba mfululizo bila kupumzika tangu
mwaka 1960, alitangaza azma ya kuachana na muziki jana wakati akiongea
na wanahabari.
Mkongwe huyo, alitaja sababu kubwa mbili za
kufikia uamuzi huo, kwanza akisema amelazimika kufanya hivyo kutokana na
umri, na pili kuwaachia vijana fursa kuendeleza fani pale alipoacha.
Alisema kutokana na umri alionao, imekuwa vigumu
kwake kwenda sambamba na kasi, mabadiliko na mahitaji mapya ya muziki
huo, hivyo kazi hiyo amewaachia vijana.
“Muziki umekuwa asili yangu kwa muda mrefu, sasa
naamua kustaafu ili kutoa fursa kwa vijana kuendelea kupiga muziki huu,”
alisema Gurumo na kuongeza: “Nimestaafu muziki, lakini nitaendelea kuwa
mshauri.”
“Kwa kipindi chote cha kusimama jukwaani
kutumbuiza, mke wangu alikuwa anakosa fursa ya kuwa na mimi kwa sababu
ya kurudi usiku wa manane kutoka kazini,” aliongeza Gurumo.
Gurumo aliyezaliwa Kijiji cha Masaki, Wilaya ya
Kisarawe, Mkoa wa Pwani, aliwataka vijana wanaokuja nyuma ya muziki wa
dansi baada ya kustaafu kwake, kuiga muziki wao ambao umeendelea kudumu
na kupendwa mpaka leo.
“Kustaafu kwangu kunakwenda sambamba na kuundwa
kamati ya kuangalia jinsi ya kunisaidia kama sehemu ya kuenzi mchango
wangu katika fani ya muziki,” alisema Gurumo.
Gurumo alianza muziki na Bendi ya Kilimanjaro
Chacha mwaka 1962, kisha Bendi za Rufiji Jazz na Kilwa Jazz kufikia
mwaka 1963. Mwaka 1964, alikuwa mmoja kati ya waanzilishi wa Bendi ya
Nuta Jazz, ambayo ndiyo ilikuwa kiini cha kuzaliwa Msondo Ngoma.
Pia alikuwa mmoja kati ya wasanii waanzilishi wa
Bendi ya DDC Mlimani Park mwaka 1987, kisha Orchestra Safari Sound
‘OSS’, na mwaka 1990 alirudi tena Msondo mpaka alipotangaza kustaafu.
|
No comments:
Post a Comment