Muungano wa Afrika sasa unataka mahakama ya kimataifa
ya ICC kusitisha kesi za Naibu rais wa Kenya William Ruto, Rais Uhuru
Kenyatta na mwandishi Joshua Arap Sang katika mahakama hiyo hadi pale
ombi lake kwa mahakama hiyo kutaka kesi hizo kurejeshwa nyumbani
kuamuliwa.
AU pia inataka Bwana Ruto na Rais Kenyatta
kuruhusiwa kuchagua vikao wanavyotaka kuhudhuria wakati wa kusikizwa kwa
kesi zao kutokana na majukumu yao ya kikatiba.
Kwenye barua iliyoandikwa kwa ICC,
AU inasema kuwa mahakama hiyo mwanzo ilipaswa kuamua ikiwa itaweza
kuhamishia kesi hizo nchini Kenya kabla ya hata kuanza kuzisikiliza.
Katika barua yake kwa ICC, AU pia Imegusia swala
la rufaa ambayo imewasilishwa katika mahakama hiyo na mwendesha mkuu wa
mashtaka Fatou Bensouda dhidi ya kumruhusu bwana Ruto kuhudhuria tu
baadhi ya vikao akisema kuwa majaji wangemlazimisha naibu rais Ruto
kuhudhuria vikao vyote vya kesi yake kabla ya rufaa kuamuliwa.
Muungano huo umeelezea kuhusu mikutano mikuu
miwili ya usalama inayotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu ambayo Rais
Kenyatta hataweza kuhudhuria kwa sababu kesi ya naibu rais William Ruto
itakuwa inasikilizwa ICC.
AU imeongeza kuwa kesi hizo zitahujumu jukumu la
Kenya katika ukumbi wa kimataifa ikisisitiza kuwa hazipaswi kuathiri
majukumu ya viongozi hao wawili.
AU inasema kuwa licha ya kuwa Kenya imekuwa ikiheshimu mahakama hiyo, inapaswa kufanya hivyo kwa kuzingatia Katiba yake.
|
No comments:
Post a Comment