|
Gaidi Samantha Lewthwaite maarufu kama ‘mjane mweupe’ raia wa Uingereza
anayedaiwa kuhusika katika tukio la shambulizi la kigaidi jijini
Nairobi, Kenya mwezi uliopita, amezua tafrani kubwa baada ya kuzuka
uvumi kuwa ameonekana katika benki moja jijini Dar es Salaam.
Mjane mweupe ni gaidi anayehusishwa na tukio la ugaidi kwenye kituo cha
biashara cha Westgate jijini Nairobi Septemba 14, mwaka huu na
anatafutwa na vyombo vya usalama vya Kenya na polisi wa kimataifa
(Interpol) kwa udi na uvumba.
Gaidi huyo anadaiwa kuwa ndiye aliyeongoza katika mashambulizi hayo
yaliyoua watu 67 na kujeruhi zaidi 200 katika kituo hicho na kufanikiwa
kutoroka kwa kujifanya kuwa mmoja watu waliokuwa wakijiokoa.
Kutokana na kutoroka kwa gaidi huyo, vyombo vya usalama katika nchi za
Afrika Mashariki vimekuwa macho kufuatilia watu ambao wanahisiwa kuwa
wanahusika na shambulizi hilo linalodaiwa kusukwa na kutekelezwa na
mtandao wa kigaidi wa al Shaabab kwa kushirikiana na Al Qaeda.
Kufuatia hali hiyo, mwanamke mmoja raia wa Uingereza, jana alikamatwa na
Jeshi la Polisi Tanzania baada ya kutiliwa shaka akifananishwa na gaidi
huyo mtukutu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo NIPASHE imezipata ambazo pia zimesambazwa
katika mitandao ya kijamii, mwanamke huyo alikamatwa katika benki ya
Exim tawi la Tower jijini Dar es Salaam baada ya wafanyakazi wa benki
hiyo kumtilia shaka.
Chanzo cha habari kutoka katika benki hiyo kilieleza kuwa mwanamke huyo
shombe alifika katika ofisi za benki hiyo makao makuu kuomba tenda ya
kusafisha jengo.
Mwanamke huyo ambaye Jeshi la Polisi bado halijataja jina lake, alifika
katika benki hiyo Jumatatu ili aonane na meneja, lakini aliambiwa aende
kesho yake yaani juzi.
Habari zinasema kuwa baada ya kufika makao makuu ya benki hiyo,
aliambiwa meneja hayupo, ndipo alipoibua hoja mpya na kuwaambia
wafanyakazi wa benki kuwa angelipenda kufungua akaunti kwenye tawi la
benki hiyo.
Baada kukubaliwa aliambiwa awasilishe nyaraka za kumtambulisha, lakini
akadai ni raia wa kigeni na hana nyaraka zozote na alipoulizwa anakaa
wapi, alidai kwenye nyumba za kupanga za Uhuru Heights.
Wafanyakazi wa benki hiyo baada ya kuona maelezo yake hayajitoshelezi,
walitoa taarifa polisi wanaolinda jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi jirani na benki hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Polisi walifika eneo hilo na kumkamata
mwanamke huyo na kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi na alipofanyiwa
uchunguzi, ilibainika alivaa lenzi kwenye macho na pia usoni alikuwa
amejipaka vitu ambavyo vilikuwa havionyeshi vizuri uso wake.
Kufuatia hali hiyo, polisi walimwamuru anawe uso na baada ya kufanya
hivyo, sura yake ya Kishombe ikapotea na kubaki kama Mzungu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Manongi, alipolizwa kuhusu tukio hilo, alisema hakuwa na taarifa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna
Suleiman Kova, alithibitisha kukamatwa kwa mwanamke huyo katika benki ya
Exim baada ya kutiliwa shaka na wananchi.
Alisema baada ya kumfanyia uchunguzi, ilibainika kuwa siyo gaidi kama
ilivyokuwa inahisiwa, badala yake na ana mume ambaye yupo jijini Dar es
Salaam.
“Huyu mwanamke ni raia wa Uingereza, alipokamatwa alikutwa amevaa hijab
na kimsingi wananchi ndiyo waliomtilia shaka, lakini siyo gaidi kama
yule anayetuhumiwa kufanya ugaidi jijini Nairobi, Kenya,” alisema Kova.
Kamishna Kova alisema mwanamke huyo aliachiwa baadaye baada ya kubainika
kuwa ameolewa na mume wake yupo Dar es Salaam.
Alisema kilichowafanya wananchi wamtilie wasiwasi ni uvaaji wake wa nguo
ambao uliwafanya wahisi huenda anafanana na gaidi wa tukio la Kenya.
Kamishna Kova alipongeza wananchi kwa jinsi wanavyokuwa makini katika
suala la ulinzi na usalama wa nchi yao kwa kuwashuku watu ambao
hawawaelewi na kuwataka kuendelea kushirikiana na jeshi hilo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Rasilimali watu wa Jeshi la Polisi,
DCP Thobias Andengenye, alitoa taarifa kuwa jeshi hilo litamsaka gaidi
Samantha Lewthwaite anayedaiwa kupitia mpaka wa Namanga mkoa wa Arusha
kabla ya kwenda kufanya tukio Nairobi ili kumzuia kufanya uhalifu zaidi.
Andengenye alikuwa akihojiwa katika kipindi cha kipima joto
kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV kilichokuwa kikijadili
Watanzania wamejifunza nini katika kuchukua hatua juu shambulio la
ugaidi lililotokea Nairobi.
Andengenye alisema Jeshi la Polisi limejipanga kumsaka gaidi huyo ili
asije akatenda uhalifu zaidi na kwamba ufuatiliaji wa mwanamke huyo
hautafanywa kwenye mipaka bali hata ndani ya nchi.
|
Habari hii imenukuliwa kama ilivyo kutoka Gazeti la Nipashe la Tanzania.
No comments:
Post a Comment