Baada ya aliyekuwa Naibu katibu Mkuu wa Chadema Zitto Kabwe pamoja na aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu wa chama hicho Dr Kitila Mkumbo kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua ya chama chao kuwavua vyeo vyao vyote ndani ya chama hatimaye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewaandikia
barua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, na aliyekuwa Mjumbe wa
Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, ambao wiki iliyopita walivuliwa nafasi za
uongozi, zinazoeleza mashtaka ya makosa 11 wanayotuhumiwa kuyatenda
dhidi ya chama hicho.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema barua
hizo, ambazo Zitto na Dk. Mkumbo, walitarajiwa kukabidhiwa jana,
zinawataka wajieleze kwa nini wasichukuliwe hatua zaidi, ikiwamo
kufukuzwa uanachama.
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam
jana, siku mbili baada ya Zitto na Dk. Mkumbo, kuitisha mkutano na
waandishi wa habari, Jumapili wiki iliyopita na kusema hadi siku hiyo
walikuwa hawajapata barua hizo zaidi ya kusikia suala hilo kwenye vyombo
vya habari.
Mnyika alisema mashtaka ya makosa, ambayo Zitto na Dk. Mkumbo
wanatuhumiwa kuyatenda, yanahusiana moja kwa moja na ukiukwaji wa
katiba, kanuni, maadili na itifaki ya chama hicho.
Alisema uamuzi wa kuwavua nafasi za uongozi ulifikiwa na Kamati Kuu
(CC) ya Chadema katika vikao vyake vilivyofanyika wiki iliyopita.
Mnyika alisema baada ya maamuzi hayo ya CC, juzi sekretarieti yake ilikutana kwa mujibu wa kazi zake za kikatiba.
Alisema ikiwa sehemu ya utekelezaji wa maamuzi ya CC, sekretarieti
ilikamilisha mapitio ya yaliyojiri pamoja na maamuzi ya CC juu ya suala
hilo pamoja na kukamilisha barua hizo kwa wahusika.
“Na naomba kuwajulisha tu kwamba, leo (jana) wahusika wote (Zitto na Dk.
Kitila) watapatiwa barua zao kwa maana kwamba barua zao ziko tayari
zinazoeleza maamuzi ya Kamati Kuu,” alisema Mnyika.
Alisema maamuzi ya CC hayakuhusu tu kuwavua uongozi, bali yalihusu
vilevile kutakiwa kuandikiwa kujieleza ni kwa nini wasichukuliwe hatua
za ziada, ikiwamo kufukuzwa uanachama kutokana na makosa waliyoyafanya
na waliyokifanyia chama.
“Na kwa kweli ni makosa waliyoyafanya na ambayo wamekifanyia chama
yalielezwa na maamuzi ya Kamati Kuu yaliyotangazwa,” alisema Mnyika.
MAKOSA YANAHUSIANA NA WARAKA
Alisema makosa hayo yalihusiana na waraka ulioandikwa, ambao kimsingi ulikiuka katiba, kanuni, maadili na itifaki ya chama.
“Sasa kwenye mashtaka yao na barua zao ambazo leo watakabidhiwa
kumeeleza mashtaka na makosa 11, ambayo watajwa wameyafanya ya kukiuka
kanuni, katiba na itifaki ya chama,” alisema Mnyika.
Alisema mashtaka waliyoandikiwa, yamejikita katika maamuzi ya CC, ambayo yalihusu waraka wa siri.
“Na siyo masuala, ambayo wahusika baada ya Kamati Kuu kupitisha maamuzi
yale wameyasema kwenye vyombo vya habari masuala ambayo siyo
yaliyoifanya Kamati Kuu ifikie maamuzi iliyoyafikia,” alisema Mnyika.
Aliongeza: “Kwa hiyo tayari wahusika wameandikiwa barua na nisisitize
kwamba, maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu ya chama yamefanywa kwa
mujibu wa katiba, kanuni, maadili na itifaki ya chama.”
Maamuzi hayo ya CC yalimvua Zitto, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini
wadhifa za Naibu Katibu Mkuu na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida.
Kwa maana hiyo, Zitto ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu (CC)
Mjumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu, amebaki kuwa mwanachama wa
kawaida.
Aidha, uongozi wa wabunge wa Chadema uliagizwa na CC kumwandikia barua
Zitto ya kumwondoa katika nafasi ya Naibu Msemaji wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni wa Wizara ya Fedha haraka iwezekanavyo kwa tuhuma za
kukisaliti chama.
Pia aliyekuwa Mjumbe wa CC, Dk. Kitila, na aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, ambao nao wamevuliwa nyadhifa
zote za uongozi na kubaki kuwa wanachama wa kawaida.
Akijibu yaliyozungumzwa na Zitto na Dk. Kitila baada ya maamuzi ya CC
dhidi yao, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema ni maneno
ya kupoteza lengo kwa kuwa walivuliwa nafasi za uongozi kwa sababu ya
waraka ule na siyo kwa sababu ya kile alichokiita uongo wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
‘Uongo’ wa PAC unaodaiwa na Lissu, ni kauli iliyowahi kutolewa na
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto akisema hakuna chama chochote cha
siasa, ikiwamo Chadema, ambacho hesabu zake zimekaguliwa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Lissu alisema hata Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatambua kuwa
Chadema ni kati ya vyama, ambavyo hesabu zake zimekaguliwa.
Alisema Chadema ina nyaraka zinazothibitisha hilo tangu mwaka 2010, 2011
na 2012, ambazo Zitto alipokuwa Naibu Katibu Mkuu alipaswa kuzijua.
Lakini alisema Zitto alishindwa kuzijua nyaraka hizo kwa sababu
alipokuwa kiongozi wa chama hakuwa na mazoea ya kufika ofisini, badala
yake amekuwa akiishia kukitungia uongo chama.
“(Zitto) Anatumia jukwaa la PAC kutukanyaga kwa hoja za uongo,” alisema Lissu.
Mbali na hilo, Lissu alisema pia kuwa Zitto na Dk. Mkumbo hawakuvuliwa
nafasi za uongozi katika chama kwa sababu ya yeye (Zitto) kukataa
kupokea posho au kuuza majimbo ya uchaguzi, ambayo Chadema ilisimamisha
wagombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Kuhusu hoja kwamba CC haina mamlaka ya kumvua mwanachama nafasi ya
uongozi bali Baraza Kuu la chama, alisema haina msingi kwa kuwa katiba
ya Chadema imeipa mamlaka CC kama itaona kuna dharura ya kufanya hivyo.
Alitoa mfano akisema mwaka 2004 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.
Amani Kabourou alivuliwa nafasi hiyo na CC. Pia mwaka 2007, CC ilimvua
Umakamu Mwenyekiti Taifa, marehemu Chacha Wangwe.
Alisema vipindi vyote hivyo, Zitto alikuwapo na alishuhudia hayo.
“Sasa kama CC ilikuwa sahihi vipindi vyote hivyo basi na sasa ni sahihi,” alisema Lissu.
Alisema mashtaka ya makosa 11, ambayo Zitto na Dk. Kitila wanatuhumiwa
kuyatenda hawawezi kuyaweka hadharani, bali watawakabidhi wahusika na
kwamba, kama wao wataamua kufanya hivyo hilo litakuwa juu yao.
Hata hivyo, alisema wanaweza kuyaweka hadharani baada ya CC kupokea utetezi kutoka kwa watuhumiwa.
Alisema mwaka 2012, Chadema ilitengeneza mwongozo unaomtaka mwanachama
kutangaza kusudio la namna ya kugombea uongozi katika chama na kwamba,
walifanya hivyo ili kuzima chokochoko zilizokuwa zimekithiri kuelekea
kwenye uchaguzi katika siku za nyuma.
Kwa mujibu wa Lissu, mwongozo huo unataka mwanachama atangaze wazi
kusudio lake hilo kwa kupeleka barua kwa Katibu Mkuu na siyo kwa
kujificha na kuchafua wengine.
“Kama wangekuwa wanataka mtu wao (awe mwenyekiti wa Chadema)
wangetangaza. Maamuzi ya Kamati Kuu ni uthibitisho kwamba hakuna
tunayemuogopa,” alisema Lissu.
Alisema ni kweli suala la PAC lilijadiliwa katika vikao vya CC, lakini halikuwa hoja ya kuwashtaki wahusika.
FEDHA ZA SABODO
Kuhusu Sh. milioni 100 zilizowahi kutolewa na mfanyabiashara Mustafa
Sabodo kwa Chadema mwaka 2009, Lissu alisema zipo kwenye ripoti ya CAG
na ile iliyopelekwa na chama kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kwamba,
hajawahi kumsikia Zitto akihoji fedha hizo na zile za ruzuku ya chama
kwenye vikao vya chama.
|
No comments:
Post a Comment