Monday, March 25, 2013

SOMA HABARI HII YA NAIBU WAZIRI KUTUHUMIWA KUTUMIA MAJINA MBALIMBALI KATIKA ELIMU YAKE.



Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo anadaiwa kutumia ujanja katika wasifu na elimu yake ambapo katika maisha yake ya kielimu ametumia majina manne tofauti. Philipo Augustine Mulugo ndiyo jina lake halisi ambalo alilisomea mpaka alipohitimu darasa la saba kwa mara ya kwanza 1988, lakini kutokana na kwamba hakufaulu kwenda sekondari alirudia darasa hilo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa takriban miezi mitatu sasa umebaini kuwa 1989, Mulugo alirudia darasa la saba katika Shule ya Msingi Rukwa ya mkoani Mbeya akitumia jina la Hamimu Hassan.

Imebainika kuwa kabla ya kuhitimu darasa la saba kwa mara ya pili, alibadili jina hilo (kutoka Hamimu Hassan) na kuwa Hamimu Augustino ambalo aliendelea nalo wakati akisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari kutwa ya Mbeya (Mbeya Day) mwaka 1990.

Hata hivyo, Mulugo mwenyewe akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam alipuuza tuhuma hizo kwa kusema kuwa ni njama za kisiasa zinazofanywa na maadui zake. Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule.

“Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo na kuongeza:

“Haya mambo kabla hata sijachaguliwa kuwa Mbunge, tulivyokuwa bado kwenye mchujo wa ndani, usiku wa manane watu walisambaza huu uvumi na nilivyoenda kwenye kikao nikatoa vyeti vyangu, wakaviona.”

Waliomfundisha

Baadhi ya walimu waliomfundisha Mulugo, watu waliofanya kazi naye pamoja na wakazi wa Kijiji cha Udinde alikozaliwa, maelezo yao yanathibitisha mabadiliko ya majina ya Mulugo kwa nyakati tofauti pia ngazi mbalimbali za kielimu.

Uchunguzi unabainisha kuwa baada ya kuhitimu kidato cha nne, alifaulu kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana, Songea ambako alisoma kati ya 1994 na 1996 akiendelea kutumia jina la Hamimu Mulugo.

Baada ya kuhitimu kidato cha sita, uchunguzi ulibaini kuwa Mulugo alirejea Mbeya na 1998 alilazimika kubadili tena jina pale alipotumia cheti cha mtu aitwaye Dickson Mulungu, kuombea kazi ya kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Southern Highlands.

Habari zinasema Mulugo alichukua hatua hiyo ili kumshawishi mmiliki wa shule hiyo mfanyabiashara, Gulnoor Dossa (sasa ni marehemu), kumpa nafasi ya kufundisha shuleni hapo.

“Mulugo alilazimika kutumia cheti cha rafiki yake aliyekuwa akiitwa Dick Mulungu ambaye alipata daraja la pili katika Shule ya Sekondari ya Songea Boys, hivyo ikawa rahisi kwake kupata kazi ya ualimu katika shule hiyo,” alisema mmoja wa waliofanya kazi naye shuleni hapo (jina tunalihifadhi kwa sasa).

Aliongeza kuwa Mulugo alianza kama mwalimu wa kawaida, lakini baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shule (headmaster) wakati hakuwa hata na cheti cha ualimu. Alichukua nafasi hiyo ya ukuu wa shule baada ya aliyekuwapo kufariki dunia.

“Unajua wale wahindi (wamiliki) walikuwa ni wafanyabiashara kwa hiyo hawakufuatilia kiwango cha elimu ndiyo maana walimpandisha tu madaraja bila kujali kuwango cha elimu,” alisema rafiki yake huyo na kuongeza:

“Nilimshauri aachane na cheo hicho kwani kama ungefanyika ukaguzi wa Serikali na kumkuta bila vyeti vya ualimu angechukuliwa hatua, hivyo alinisikiliza na akaachia nafasi hiyo na kujipa cheo cha umeneja wa shule.”

Suala la uwezo na elimu ya Mulugo liliibua mjadala siku chache zilizopita baada ya kutoa kauli nchini Afrika Kusini aliponukuliwa akisema Tanzania ni muungano wa nchi mbili ambazo ni Tanganyika na Zimbabwe badala ya Zanzibar.

Alikotokea

Uchunguzi wa gazeti hili ulianzia katika kijiji alichozaliwa cha Udinde, Kata ya Kapalala wilayani Chunya mkoani Mbeya na alisoma Shule ya Msingi ya Rukwa.

Mmoja wa walimu waliomfundisha aliyejitambulisha kwa jina la Nyoni anasema anakumbuka kwamba Naibu Waziri huyo 1989 na wakati huo alikuwa akijulikana kwa jina la Hamimu Hassan.

“Mimi nilihamia hapa 1989 nikitokea Shule ya Msingi Kapalala. Kulikuwa na mwalimu mmoja tu kwa hiyo nikawa wa pili. Namfahamu Mulugo wakati huo akiitwa Hamimu Hassan. Sijui kabla hapo alikuwa akitumia jina gani,” alisema Nyoni anayetarajia kustaafu kazi ya ualimu mwakani.

Mmoja wa ndugu wa karibu wa Waziri Mulugo anayeishi kijijini hapo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alikiri kuwa awali waziri huyo alikuwa akiitwa Philipo Augustino Mulugo.

“Philipo amesomea hapo Rukwa, ambayo ni Shule ya Msingi na alikwenda Kijiji cha Mkulwe kabla ya kwenda Mbeya kuwa Mwalimu. Sijui kama alirudia shule,” alisema ndugu huyo.

Mkazi mwingine wa kijijini hapo, Peter Kayuti alikiri kumfahamu Waziri Mulugo tangu enzi za utoto na kwamba alirudia darasa la saba, lakini alisema hakumbuki jina la pili alilolitumia. “Ni kweli Philipo alirudia shule, lakini sijui kama alitumia jina jingine zaidi ya hilo la sasa,” alisema Kayuti.

Mwalimu aliyemfundisha katika Shule ya Sekondari Mbeya ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe, alikiri kumfahamu kwa jina la Hamimu Augustino, lakini akasema hafahamu lilibadilika lini.

“Ni kweli, nilimfundisha Waziri Mulugo na alikuwa akiitwa Hamimu Agustino. Sidhani kama ni jambo geni kwa wanafunzi hasa wa zamani kurudia shule… Zamani ilikuwa kawaida kwa kuwa shule zilikuwa chache. Sijui alibadilisha jina hilo lini, lakini hilo ni suala la kisheria tu,” alisema mwalimu huyo.

Utata wa majina

Mwalimu mwingine aliyewahi kufanya kazi na Waziri Mulugo katika Shule ya Southern Highlands alisema waziri huyo alikuwa na tabia ya kuchanganya majina yake ya awali ili kuficha cheti alichoombea kazi.

“Yule alikuwa mjanja sana, ndiyo maana ukiangalia kadi zake zilikuwa na majina mengi tu na yana badilika. Leo atasaini barua kwa jina hili kesho lile. Mara utaona ameandika kifupisho cha PHDA, yaani Philip Hamimu Dick Agustino, mara Mulungu EDM, mara Mulugu D. Philip,” alisema mwalimu huyo na kuongeza:

“Amekuwa akijaribu kulibadilisha jina la Mulungu kuwa Mulugu mwisho amelipeleka kuwa lake la awali la Mulugo. Yote hayo ni kuficha tu ukweli kwamba alitumia cheti cha Dick Mulungu,” alisema mwalimu huyo.

Mmoja wa wakuregenzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (jina tunalihifadhi) alisema: “Ili mwalimu wa sekondari awe headmaster (mkuu wa shule) ni lazima awe na shahada ya kwanza kutoka kwenye chuo kikuu kinachotambulika. Anatakiwa pia kuwa na uzoefu wa kazi wa miaka isiyopungua minane.”

Kuhusu kughushi vyeti mkurugenzi huyo alisema, ikigundulika kuwa mwalimu ameghushi cheti anafukuzwa kazi mara moja, lakini alikiri kwamba katika shule binafsi inawezekana walimu wasio na sifa wakapenya, lakini wakaguzi wakibaini hutoa maelekezo wafukuzwe.

“Kwanza siku hizi ili mwalimu aajiriwe ni lazima akabidhi vyeti vyake wizarani na hupelekwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) ili kuhakikiwa. Zamani ukaguzi haukuwa makini kwa hiyo inawezekana kuna watu wasio na sifa walipenya,” alisema.

Kuhusu kurudia darasa la saba, alisema sheria haijawahi kuruhusu watu kurudia darasa la saba na kwamba wale waliorudia hutumia mbinu zao kufanya hivyo.

“Sheria haijawahi kuruhusu watu kurudia darasa la saba. Ni kweli wengi wamerudia sijui wanatumia mbinu gani, lakini hairuhusiwi. Ukishafanya mtihani wa darasa la saba mara moja ndiyo basi,” alisema mkurugenzi huyo.

Msemaji wa wizara hiyo, Mtandi Bunyanzu kwa kila swali aliloulizwa alisema hana uhakika hivyo asingeweza kutoa jibu lakini kwa suala la kughushi vyeti, alisema ni kosa la jinai siyo kwa walimu tu bali kwa kila mtu atakayebainika.

“Kughushi vyeti ni kosa la jina siyo kwa walimu tu, hata waandishi wa habari,” aliongeza Bunyanzu.

Kwa upande wake, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) halikuwa tayari kutoa matokeo ya mitihani ya Mulugo na badala yake msemaji wa baraza hilo John Nchimbi alisema matokeo hayo ni siri ya mtahiniwa na hawezi kupewa mtu mwingine.


No comments:

Post a Comment