MBUNGE wa Kinondoni
(CCM), Idd Azzan, amesema yupo tayari kujiuzulu ubunge, ikiwa
itabainika anajihusisha biashara ya dawa za kulevya. Kauli hiyo imekuja
siku chache baada ya kutajwa katika moja ya barua iliyosambazwa katika
mitandao ya kijamii, baada ya mtu anayedaiwa kukamatwa China na
kuwatuhumu watu kadhaa akiwamo Idd Azzan.
Akizungumzia kuhusu sakata hilo jana, alisema hatua ya kuhusishwa na
biashara haramu ya dawa za kulevya, ni kutotenda haki mbele ya jamii
hasa wapiga kura wake na Taifa kwa ujumla.
Alisema mtu aliyendika barua ya tuhuma dhidi yake, ni wazi amedhamiria
kumshushia heshima na huenda akawa ana jambo limejificha.
“Ni kweli nimeiona hiyo barua katika mtandao, inayodaiwa imeandikwa na
kijana ambaye amekamatwa Hong Kong nchini China. Lakini ninajiuliza
kama kweli yeye ni raia mwema, katika hili kwanini hakutaka kutaja jina
lake kwenye barua hiyo.
“Hata nilipoisoma nimebaini kuwa huyo mtu ametumika na huenda kabisa
hayupo nje ya nchi, kwani katika maelezo yake anataja jina la Balozi
Philip Marmo kuwa amemsaidia hali ya kuwa hivi karibuni Rais Kikwete
alimteua Balozi mpya Abdulrahman Shimbo na Marmo kuwa Balozi wa
Shirikisho la Ujerumani.
“Kingine naona alijaribu kuandika uongo kuweza kuaminisha jamii, kwani
hata hilo jila la balozi mwanzo limetajwa jina la Bernad na kukatwa
kwa wino. Ninapenda kulieleza Taifa kuwa naomba vyombo vya usalama
vifanye uchunguzi wa jambo hili na nikibainika ninauza dawa za kulevya
nipo tayari kujiuzulu ubunge wangu.
“Kubwa haki itendeke katika kufanya uchunguzi wa jambo hili, ila ni
lazima jamii na Watanzania kwa ujumla tusikubali kwa makusudi watu
waichafue nchi yetu kwa chuki na fitna tu,” alisema Azzan.
Alisema kutokana na hali hiyo, anashindwa kuchukua hatua yoyote ya
kufanya zaidi ya kuliandikia barua Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi
dhidi ya barua hiyo kuweza kubaini ukweli wa jambo hilo.
“Sijawahi kuuza dawa za kulevya na hata katika familia yangu hakuna
mtu anayefanya biashara hiyo haramu. Kila mmoja anajua kuwa Idd
nilikuwa Diwani wa Kata ya Magomeni, huku kazi yangu kubwa ikiwa ni
biashara ya magari na daladala ambayo ninaendelea nayo hadi sasa mbali
ya ubunge kama nilivyopewa heshima na wapiga kura wangu wa Kinondoni,”
alisema Azzan.
Alipoulizwa kuwa ni hatua gani ikibainika hakuna ukweli wa jambo hilo
baada ya vyombo vya usalama kufanya uchunguzi, alisema atakachokifanya
anamuachia Mungu.
“Ni ngumu kusema hatua gani nitachukua ikibainika hakuna ukweli,
lakini nataka kusema kama yule aliyeandika barua hii angetaja jina lake
ni wazi baada ya uchunguzi ningeweza kuomba ushauri kwa mwanasheria
wangu hatua za kuchukua, lakini kwa kuwa hakutaja jina ni ngumu kuweza
kuamua,” alisema Azzan.
Kwa mujibu wa taarifa zilitolewa kupitia mitandao, ziliripoti kukamatwa
kwa Watanzania wawili nchini China wakiwa na dawa za kulevya zenye
thamani ya Dola milioni 3.34 za Marekani. |
No comments:
Post a Comment