|
Jeshi
la Wananchi, Polisi, Uhamiaji na vyombo vingine vya usalama pamoja na
baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara maarufu nchini wametajwa
kujihusisha na biashara haramu ya madawa kulevya ambayo imeharibu maisha
ya maelfu ya vijana na kuvunja vunja familia. Taarifa za kuhusika huku
kwa maafisa wa vyombo hivi vya usalama na watu hawa mashuhuri zimekuja
baada ya mmoja wa vijana wa Kitanzania aliyekamatwa huko Hong Kong
kuandika barua ya kukiri kuhusika kwake na bishara hiyo pamoja na
kuwataja watu waliomuingiza na kumwezesha kufanya biashara hiyo.
Barua hiyo ilipostiwa katika mojawapo ya tovuti zinazofuatilia mambo
ya madawa ya kulevya na kubandikwa chini ya kichwa cha habari cha
“Punda wa Madawa” kwenye mtandao wa waumini wa Kanisa Katoliki ambao
umeundwa ili kuunga mkono mabadiliko na mafundisho ya Mtaguso wa Pili
wa Vatikano.
“Punda wa Madawa” ni jina linaloelezea watu wale wanaotumiwa na
kutumika kusafirisha madawa ya kulevya kutoka kwa wafanyabiashara wa
jumla kwenda kwa wafanyabiashara wa reja reja. Watu hawa wanaweza kuwa
ndani ya nchi au kati ya nchi na nchi. Mara nyingi – kama jina
linavyoashiria – watu hawa ni vyombo tu vya vinara wa madawa wa kulevya
na lolote litakalowakuta huwa ni juu yao wenyewe. Hata hivyo, endapo
wanafanikiwa kusafirisha ‘mzigo’ kutoka pointi moja kwenda nyingine
basi huweza kulipwa vizuri na wengine huishi maisha ya kifahari kabisa
kutokana na biashara hii.
Kabla ya kwenda kuwataja watu ambao mwandishi anawatuhumu kujihusisha
na biashara hii mtunzi wa barua hii anaelezea kwa kirefu jinsi
alivyoingia katika mtego wa kujihusisha na biashara hiyo na hatimaye
kujikuta akiangukia kwenye mikono mikali ya sheria ya polisi wa Hong
Kong, China. Mwandishi anaelezea kwa kirefu kuwa aliingia katika
biashara hiyo baada ya shida za maisha kumzidia na kujikuta hana njia
ya kupata kipato kingine halali ili kuisaidia familia yake na hivyo
kuamua kutumia njia za mkato.
“Pamoja na misukosuko yote hiyo nilivumilia, lakini mtihani mkubwa ni
pale kodi ya nyumba ilipoisha na mwenye nyumba akanipa notice ya mwezi
mmoja (nihame), au nimpe kodi ya miezi ya 360,000tsh” ameelezea
mwandishi huyo ambaye hakuweka jina lake. Mwandishi huyo wa barua
anadai kuwa baada ya kujitahidi kutafuta fedha hiyo na kushindwa
alijikuta ameomba msaada kwa marafiki zake ambao anawaita ‘wabaya’
kwani ni wao ndio walimchukua na kumpeleka kwa bosi wao ambaye
alimlipia kodi ya miezi sita na kumpa fedha za ziada za shilingi laki
mbili. Tajiri huyo ni mtu anayeishi Magomeni Mwembechai.
Ni hapo ndipo alipoanza kupewa mazoezi ya kumeza vidonge vya heroin.
Siku chache baadaye alijikuwa amepewa vidonge 93 vya madawa hayo
ambavyo kila kimoja kina gram 15 kwa jumla ya gram 1395 (sawa na paundi
tatu hivi-MM). Kutokana na kuanza kupata matatizo na kutoka vidonda
kijana huyo alijaribu kutaka kuacha biashara lakini akakumbushwa kuwa
ana deni la 560,000Tsh na upande mwingine aliahidiwa kuwa endapo
angefikisha mzigo ule salama basi angelipwa dola 5000. Akapewa mpango
wa safari kwenda Hong Kong akiwa katika hali ya udhaifu mkubwa wa
mwili.
Mwandishi alitarajia kuwa kutokana na hali mbaya basi wangekamatwa
uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar. Hiyo haikuwa hivyo kwani
kwa maelezo yake “Ajabu pale airport kulikuwa na mtu ambaye
aliandaliwa kunipitisha mimi mpaka boarding room” anasema kijana huyo.
Ilikuwa ni hali aliyokuwa nayo ndiyo iliwafanya maafisa wa Hong Kong
kumtilia shaka na kumweka kizuizini.
Kitu ambacho mwandishi inaonekana hakuwa anakijua ni kuwa Hong Kong
hawana huruma na watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya kwani wana
vifungo vikali kabisa na kwa maelezo yake kuwa hadi hivi sasa kuna
vijana wa Kitanzania karibu 150 ambao wameshafungwa na wengine
wakiendelea kusubiri kesi zao ziendelee. Alichoshukuru Mwandishi ni
kuwa angalau yeye na wenzake wamekamatwa Hong Kong kwani kama
wangekamatwa China yenyewe basi wangenyongwa kwani tayari – kwa maelezo
yake – wapo vijana wa Kitanzania walionyongwa huko.
Kwa maelezo yake ambayo yanashabihiana kwa kiasi kikubwa na taarifa za
vyombo vya usalama vya kimataifa vinavyofuatilia biashara hii haramu
mizigo ya madawa ya kulevya yanaingia nchini Tanzania yakitokea
Pakistani na Afghanistan kupitia maeneo ya Tanga, Dar, Mtwara na
Bagamoyo ambayo huja kwa boti na kupokelewa na wahusika wakubwa nchini.
Ikumbukwe kuwa mwaja jana Januari mtoto wa aliyekuwa afisa wa Benki
Kuu Amatus Liyumba aitwaye Morine alikamatwa na wenzake huko Lindi
akiwa na mzigo wa madawa ya kulevya wenye thamani ya zaidi ya dola
bilioni 9!
“Mizigo hiyo huwa inasindikizwa na magari ya jeshi na polisi na hii
siyo siri kwani hata wahusika wanajua” amesema kijana huyo katika barua
hiyo ambayo imewashtua Watanzania wengi baada ya kupostiwa katika
mtandao maarufu wa JamiiForums siku ya Jumamosi.
Kuhusishwa kwa vyombo vya usalama na biashara hii haramu si jambo la
kushangaza kwa watu ambao wamekuwa wakifuatilia kuenea kwa vitendo vya
uhalifu nchini. Ipo mifano kadha wa kadha ambayo inaonesha kuwa baadhi
ya watumishi wa vyombo hivi vya usalama wako ‘compromised’ na
haijulikani ni nani anaweza kuaminika. Baadhi ya mifano ni hii
ifuatayo:
- ·
Mwaka 2011 – Mwanajeshi wa JWTZ alikamatwa mjini Morogoro
akijaribu kusafirisha magunia 12 ya bangi kutoka Iringa kuja Dar. Hii
ilikuwa ni mwezi Disemba mwaka huo. Kijana huyo wa miaka 26 alikamatwa
na askari wa polisi waliokuwa doria akiwa amevaa sare za jeshi hilo. Ni
afisa wa Kambi ya Lugalo mwenye namba MT86879.
- ·
Januari 2013 – Afisa wa JWTZ mwenye namba MT 59503 Sajenti Aziz
Athumani alikamatwa huko Arusha akiwa na pembe mbili za ndovu.
- Aprili
2013 - Askari wa Magereza Brighton Octavian alikamatwa katika gereza la
keko akiwa na kete 732 ambazo inadaiwa alikuwa anazipitisha kwenda kwa
wafungwa. Kuna ushahidi mkubwa wa uwepo wa mtandao wa kihalifu wa
maafisa wa magereza ambao wamekuwa wakitumiwa na wafungwa kupeleka
habari nje au kuleta habari ndani kutoka kwa mabosi wa madawa ya kulevya
nchini.
- ·
Julai 2013 – Hivi majuzi tu mwanajeshi mwingine Seleman
Chasama (50) –katika hali ya kushangaza akili kabisa – amefikishwa
mahakamani akishtakiwa makosa ya uhujumu uchumi na yale ya Uhifadhi wa
Wanyama Pori baada ya kukutwa na pembe 357 za ndovu zenye thamani ya
dola milioni 2.6.
- ·
Julai 2013 – kabla hilo la mapema Julai halijatulia wiki
iliyopita taarifa za maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza kukamatwa
na nyara za serikali nalo zimeonesha kuwa hata Magereza nako si salama.
Maafisa hao akiwemo Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Joseph Sauli,
Warden Richard Barick na Koplo Silvester Bukha walikutwa wakitumia gari
la Magereza kubeba Twiga 2, Pundamilia 2, Swalapalapala 2 na Mbuni 2
wote wakiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 55!
Hiyo ni mifano michache tu ya kuhusishwa kwa maafisa wa usalama na
mambo ya ujangili, madawa ya kulevya na hapo hatujaangalia uhalifu
mwingine. Na hapa izingatiwe hawa ni wale ambao walikamatwa tu na
hatujaangalia wale wa polisi ambao kama watu wanakumbuka waliwahi
kutuhumiwa kujaribu kumtegeshea mtoto wa Mzee Mengi madawa ya kulevya
pale Uwanja wa Ndege na barua hii inatupa mawazo tu jinsi gani hilo
linaweza kutokea kweli.
Ikumbukwe barua hii imekuja tayari kukiwa na habari za mabinti wawili
wa Kitanzania wamekamatwa Afrika ya Kusini baada ya kutua nchini humo
na mzigo wa madawa ya kulevya wenye thamani ya zaidi ya shilingi
bilioni 6; na hawa waliondokea uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere
jijini Dar-es-Salaam. Bila ya shaka kuna kuhusika kwa maafisa wa kikosi
cha uhamiaji ambao wanawajibu wa kusimamia watu wanaoingia na kutoka
nchini.
Vilevile, barua hii imekuja siku chache tu toka Mbunge wa Musoma Mjini
Vicent Nyerere (CHADEMA) kuzungumza na waandishi wa habari kutaka
serikali ijisafishe kwani inaonekana kuwaogopa vinara wa madawa ya
kulevya. Katika tamko lake la Julai 19 Bw. Nyerere ambaye pia ni Waziri
Kivuli wa Mambo ya Ndani alisema kwa ukali kuwa “Kupuuzia na
kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za kulevya ni kuangamiza nguvu
kazi ya taifa. Nguvu kazi ya taifa ikishaharibiwa na dawa za kulevya
hatuna taifa tena. Hivyo Serikali ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia
macho jambo hili kwa manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu taifa
na huo ni usaliti dhidi ya kiapo ilichokula cha kulitumikia taifa na
kusimamia usitawi wa wananchi wa Tanzania. Aidha, Serikali itambue pia
kwamba kuendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua yoyote juu ya jambo
hili kunatoa dalili kwamba yamkini ya yenyewe inahusika na biashara
hiyo.”
Katika kuhitimisha barua yake, mwandishi wa barua hiyo alienda na
kuwataja baadhi ya watu ambao wanahusika na mtandao wa madawa ya
kulevya na namna ya ushiriki wao huku akisema kuwa wapo wengine ambao
majina yao yakitajwa nchi itashtuka kwani ni watendaji wa ngazi za juu
serikalini. Kwa mujibu wa kijana huyo wanaodaiwa kuhusika na biashara
hiyo nchini ni hawa wafuatao (kama alivyoandika):
- 1. Beka Rangers – Yupo Magomeni Mapima na ana Bureau De Change, Magomeni.
- 2. Yasin
– Yupo Sinza Madukani na amepanga floor nzima ya gofoa lililopo hapo
madukani. Ana semitrailer za kusafirishia mizigo. Anajulikana sana.
- 3. Chonji – Yupo Magomeni Mwembechai na ana ghorofa analijenga hapo Mwembechai la ghorofa tano. Naye ni maarufu sana.
- 4. Ahmed Horohoro – Maarufu hapo Magomeoni Mapipa
- 5. Gatuso – Maarufu Magomeni Mapipa – Chipolopolo
- 6. Manganja
– Sinza Uzuri Darajani. Ukitokea Magomeni kwenda Sinza –Uzuri baada
tu ya kumaliza daraja, nyumba ya pili kushoto ndipo kuna ofisi yake.
- 7. Gasper – Vijana Kinondoni; ana ofisi ya stationery hapo vijana ni maarufu sana.
- 8. David Kanyau – Anajulikana hata na maaskari wengi.
- 9. Kogoko – Yupo Dar-es-Salaam, mizigo mingi inayoenda China ni ya kwake; maaskari wanamjua sana.
- 10. Mhe. Iddi Azzan – Magomeni – Huyu ni mbunge na asichanganywe na Musa Azzan “Zungu”.
- 11. Tanaruza – Mwembechai
- 12. Shikuba – tajiri mkubwa, serikali inamtambua.
- 13. Wanaopokea mizigo huko China ni watu aliowataja kwa majina ya Omary na Shakur.
Barua yake hiyo ilitumwa kwa vyombo mbalimbali vya habari vya
Tanzania. Kitu kimoja ambako kiko wazi ni kuwa kijana huyo amefanya
kile ambacho watu wengi wameshindwa kukifanya japo wakiwa na uwezo wa
kukifanya.
Kukithiri kwa biashara ya madawa ya kulevya nchini kunafichua tu ya
kile kinachoendelea na kusukuma ‘gurudumu la maendeleo’ nchini ambapo
wakati watu wengine wanahenyeka kila siku kufanya kazi halali na kwa
jasho lao lipo kundi ambalo limejikita hadi kwenye madaraka ambalo
licha ya kufanya vitendo vya ufisadi serikalini lipo pia kwenye mtandao
wa uhalifu (organized crime) na limejipenyeza hadi kwenye vyombo vya
dola. Barua ya kijana huyu kuhusisha vyombo vya usalama yaweza kuwa ni
andiko la mwisho kwa serikali ya Kikwete kuangalia utendaji wa vyombo
vyake ambavyo anaonesha kuwa anaviamini sana.
Jambo la kutisha ni kuwa kutokana na watu wa makundi mbalimbali
kuhusishwa na biashara ya madawa ya kulevya tusije kushangaa hakuna
mtu yeyote ambaye tunaweza kumwamini tena. Je, serikali itapokeaje
taarifa hii? Je, kuna mtu mwenye ujasiri wa kupambana na kuufumua
mtandao huu? Je, kama kijana huyu kawafanyia kazi yote na kuwatajia
majina na mahali je serikali ya Tanzania ina maana kuwa miaka yote hii
haijui watu hawa na kama haiwajui vyombo vya usalama kwanini vinatumia
“intelijigensia” nyingi kwenye mikutano ya CDM badala ya wahalifu hawa
wakubwa? Na kama watu hawa waliotajwa hawajulikani na vyombo vya
usalama au wanajulikana lakini hawakamatwi je Kikwete anahalalisha vipi
kuendelea kuwatumia watu wale wale walioshindwa kusimamia usalama wan
chi? Si ni yeye aliyesema jusi kwenye sikukuu ya mashujaa kuwa nchi iko
“salama”. Kama yaliyomo kwenye barua hiyo ni kweli je tunaweza kusema
kweli nchi iko “salama”? Salama kwa nani?
Maswali 2 ya kujiuliza na kufikirisha:
1. Kwa kila madawa yanayokamatwa na kwa kila watuhumiwa wanaokamatwa ni
wangapi wanafanikiwa kupita na kuishia mitaani au nchi jirani?
2. Je, majina ya hawa waliotajwa yamo kwenye ile orodha aliyopewa Rais
Kikwete, au ile ya viongozi wa makanisa au ile ya Kikosi cha Kuzuia
Madawa ya Kulevya?
|
Makala hii ni kwa Hisani ya
/www.mwanakijiji.com
No comments:
Post a Comment