Papa Francis amethibitisha uamuzi wa kumtangaza kuwa mtakatifu mwenyeheri Yohane Paul ll ambaye alifariki dunia mwaka 2005.
Papa Francis ameeleza
kuwa miujiza mbalimbali na ushahidi wa matendo ya mwenyeheri Yohane Paul
II yanampa nafasi ya kumtangaza mtakatifu kulingana na kanuni za Kanisa
Katoliki.
Uamuzi huo wa kumtangaza mtakatifu Yohane Paul ll
utamfanya Papa Francis kumweka katika orodha ya watakatifu kiongozi huyo
ambaye aliongoza kanisa hilo tangu mwaka 1978 pamoja na Papa mwingine,
Yohane XXlll, ambaye alifariki dunia miaka 50 iliyopita na ambaye
alikuwa kipenzi cha wengi.
Kwa mamlaka yake, Papa Francis atamtangaza pia
Papa Yohane XXlll kuwa mtakatifu, ingawa makao ya kanisa hilo, Vatican
hayathibitishi rasmi muujiza wake.
Vatican ilieleza jana kuwa Papa Francis anao uwezo
na mamlaka ya kumtangaza mtu yeyote kuwa mtakatifu kufuatana na
mchakato ambao umewekwa na kanisa hilo na kwa kuzingatia vigezo
vilivyowekwa, bila kuangalia au kuegemea zaidi kigezo cha muujiza.
Hata hivyo, Vatican inaeleza kuwa sherehe za
kumtangaza mwenyeheri Papa Yohane Paul ll kuwa mtakatifu zitafanyika
kabla ya mwisho wa mwaka.
Tayari, Desemba 8 imeandaliwa rasmi kama siku
maalumu ya kufanyika kwa shughuli hiyo, kutokana na kuwa sikukuu kubwa
ya kanisa hilo kwa kumbukumbu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili,
siku ambayo pia watawa hasa wa kike huweka nadhiri zao.
Vyombo vya habari vya Poland alikozaliwa
mwenyeheri Papa Yohane Paul ll vimeendelea kueleza kuwa Oktoba ndiyo
unaoweza kutumika kwa shughuli hiyo, siku ambayo ni ukumbusho wa
kuteuliwa kwake kuwa kiongozi wa kanisa hilo mwaka 1978.
Hata hivyo, maofisa wa Vatican wameeleza kuwa itakuwa mapema mnno kwa shughuli hiyo kubwa kwa kanisa hilo.
Msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi
alithibitisha kuwa muujiza wa kwanza wa mwenyeheri Papa Yohan Paul ll
ulihusisha mwanamke raia wa Costa Rica.
Gazeti la Kikatoliki la Hispania, La Razon
limemtaja mwanamke huyo kuwa Floribeth Mora na kueleza kuwa alikuwa
akisumbuliwa na matatizo ya ugonjwa wa kichwa, ambao ulipona kwa maajabu
Mei Mosi, 2011 , siku ambayo tukio la kutangazwa kwa Yohane Paul ll
kuwa mwenyeheri kulifanyika mbele ya waumini 1.5 milioni katika Viwanja
vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa heshima yake.
Katika matoleo kadhaa ya gazeti hilo mwezi
uliopita, La Razon limeeleza kuwa Mora aliamka akiumwa kichwa Aprili 8
na kwenda hospitali, hali yake ilikuwa mbaya kiasi cha kurudishwa
nyumbani na kuambiwa kuwa ataishi kwa mwezi mmoja.
|
No comments:
Post a Comment