Maadhimisho ya miaka 95 tangu kuzaliwa kwa Mandela
yanabeba uzito mkubwa kuliko maadhimisho mengine yaliyotangulia kwani
kwa siku 40, wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa katika wasiwasi mkubwa
hasa kutokana na kuzorota kwa afya ya kiongozi huyo.
Leo, Rais Jacob Zuma atawaongoza mamilioni ya wananchi wa Afrika
Kusini katika maadhimisho ya nne ya kimataifa ya ‘Siku ya Mandela’
ambayo yanakwenda sambamba na siku yake hiyo ya kuzaliwa.
Tangu kulazwa kwa Mandela huko Pretoria, Rais Zuma
amekuwa akiwahimiza wananchi wake wajiandae kusherehekea miaka 95 ya
Mandela akiwatia moyo wale waliokuwa na wasiwasi kwamba Madiba
asingeweza kuifikia leo kutokana na matatizo ya kiafya.
Siku ya Mandela huadhimishwa kuenzi kazi za
kiongozi huyo alizozifanya kwa miaka 67 akiutumikia umma wa wananchi wa
Afrika Kusini, zikiwamo vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kuwa
Rais wa kwanza mzalendo kwa miaka mitano, kisha kustaafu.
Pia ‘Mandela Day’ hutumika kukumbuka kampeni yake
dhidi ya ubaguzi wa rangi na utetezi wa haki za binadamu maarufu kwa
jina la “46664”, ambayo ni namba ya utambulisho aliyoitumia alipokuwa
mfungwa katika Gereza la Visiwa vya Robben.
Kwa maana ya Siku ya Mandela ambayo pia
imeidhinishwa na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, wananchi wa Afrika
Kusini wanatumia dakika 67 kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa
ni hatua ya kuenzi kile wanachokiita ‘kazi za mtu aliyejitoa maisha yake
kwa ajili ya kupigania haki na utu’.
Dakika hizo 67 zinawakilisha idadi kama hiyo ya
miaka ambayo Mandela alitumika, hivyo Waafrika Kusini watakuwa wakitoa
msaada na huduma kwa jamii iwe ni kwa watoto yatima au watu wengine
ambao ni wahitaji katika jamii.
Kituo cha Kumbukumbu ya Mandela kimewataka
wananchi kuungana na kuonyesha ushirikiano wao kwa Mandela kwa kutumia
dakika 67 za muda wao kuzisaidia jamii zao ili kumuenzi kiongozi huyo
ambaye ni alama ya dunia.
No comments:
Post a Comment