Baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kufanya ziara ya kushutukiza katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA)baada ya kuwa uchochoro wa
kupitishia dawa za kulevya, umeanza kuzaa matunda baada ya mtu mmoja
kukamatwa akiwa na pipi 86 na misokoto 34 ya bangi.
Kukamatwa kwa dawa hizo kumekuja saa kadhaa baada ya Dk. Mwakyembe,
kufanya ziara ya kushtukiza katika uwanja huo na kubaini kuwa JNIA
kufanywa uchochoro wa kupitishia dawa za kulevya tatizo siyo ukosefu wa
vifaa bali ni wafanyakazi wenyewe waliopewa dhamana ya kuusimamia.
Waziri Mwakyembe alifanya ziara hiyo juzi alfajiri na mtuhumiwa wa kusafirisha dawa alikamatwa siku hiyo hiyo saa 2:15 usiku.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Dk.
Mwakyembe alimtaja aliyekamatwa kuwa ni Leonard Jeremiah Monyo (Pichani juu) ambaye
alikamatwa juzi katika uwanja huo akisafirisha dawa za kulevya aina ya
Heroen kwenda Italia kupitia Zurich, Uswisi.
Alisema mtu huyo ambaye ni raia wa Tanzania, alikamatwa katika uwanja
huo baada ya kufanyiwa ukaguzi na wanawake wawili ambao ni wafanyakazi
wa JNIA kubaini kuwa alikuwa amezificha dawa hizo katika begi lake.
Naye Kamanda wa Polisi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA),
Deusdedit Kato, alisema mtuhumiwa huyo alipokuwa anataka kupita getini,
mashine maalum za kukagulia zilibainisha kwamba alikuwa na kitu, na
hivyo askari waliokuwapo hapo walimtilia shaka na kumweka pembeni kisha
kumkagua na kumkuta na dawa hizo.
Kato alisema kuwa mpaka sasa bado hawajajua thamani ya dawa hizo ambazo
watazipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kupata uthibitisho zaidi
iwapo ni dawa za kulevya au la.
Kwa mujibu wa Kato, mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa na Polisi na
kwamba muda wowote kuanzia jana walitarajia kumfikisha katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka baada ya kupata majibu kutoka
kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.PICHA KWA HISANI YA ITV DAIMA.
|
No comments:
Post a Comment