Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu
umesema hauna imani na tume iliyoundwa na jeshi la polisi nchini
kwa ajili ya kuchunguza tukio la kupigwa risasi kiongozi wa kidini
Sheikh Ponda Issa Ponda.
Mratibu wa mtandao huo Onesmo Ole Ngurumwa amewaambia waandishi wa
habari mjini Dar es Salaam leo kuwa jeshi hilo halina haki ya kujiundia
tume ikiwa lenyewe ndiyo linatuhumiwa kumpiga risasi sheikh huyo.
Ngurumwa amesema kuwa inasikitisha
kuona vyombo vya dola vinaendelea na uvunjaji wa sheria kwa kutumia
nguvu inayokiuka haki za msingi za binadamu.
Msemaji wa Jeshi la polisi nchini Advera
Senso alisema kuwa jeshi lake kwa kushirikiana
na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya
uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi
na polisi.
Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa
kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe, hatua
iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata
hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa kidini.
Mapema Jumatatu asubuhi Baraza la waisilamu
Tanzania-BAKWATA limeunga mkono kauli ya Jumuiya ya taasisi za kisilamu
na kuitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio lililosababisha kupigwa
risasi kwa Katibu huyo wa Shura ya Maimamu nchini humo.
Kaimu Sheikh Mkuu wa Tanzania Alhad Mussa Salum
amezungumza na waandishi wa habari Mjini Dar es Salaam na kusema kuwa
japokuwa BAKWATA imekuwa ikipingana na misimamo ya Sheikh Ponda limesema
serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata Ponda kwa kufuata mkondo wa
sheria.
Sheikh Ponda amekuwa katika mivutano ya mara kwa
mara na serikali ya Tanzania, anadaiwa kupigwa risasi baada ya kutokea
vurugu kwenye mkutano wa mawaidha ya baraza la sikukuu ya Idd el Fitr
Jumamosi jioni.
Awali siku ya Jumapili Mwenyekiti wa Shura ya
Maimamu Tanzania, Alhajj Mussa Kundecha, aliwaambia waandishi wa habari
mjini Dar es Salaam kuwa endapo serikali haitachukua hatua
itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na
serikali ya nchi hiyo.
Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya Taifa,
Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la risasi huku akiwa
chini ya ulinzi wa askari kanzu.
Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi
Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi
wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi,
alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya
kilomita 200.
Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje
cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya kukutwa na
makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu.
|
No comments:
Post a Comment