|
Marekani imeongeza mda wa kufungwa kwa balozi 19 pamoja na ofisi zake za ujumbe wa kidiplomasia hadi tarehe 10 Agosti.
Idara ya maswala ya kigeni nchini humo imesema hatua hio ni ya tahadhari.
Takriban ofisi 22 zenye ujumbe wa
marekani wa kidiplomasia zilifungwa kwa mda siku mbili zilizopita mbali
na kutolewa tahadhari kwa raia wa taifa hilo kutozuru maneo ya mashariki
ya kati pamoja na kazkazini mwa afrika.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema kuwa
kufungwa kwa balozi hizo ni kutokana na serikali kuchukua tahadhari
kubwa na wala sio jibu lake kwa tisho jipya la mashambulizi.
Uingereza ilisema kuwa Ubalozi wake nchini Yemen
utasalia kufungwa hadi mwishoni kwa sherehe za siku kuu ya IDD siku ya
Alhamisi na kufunguliwa siku ya Jumanne.
Wakati huohuo, balozi za Marekani katika miji ya
Algiers, Kabul na Baghdad ni miongoni mwa zile zitakazofungwa na
kutarajiwa kufunguliwa Jumatatu wiki ijayo.
Lakini duru za kidiplomasia katika miji ya Abu
Dhabi, Amman, Cairo, Riyadh, Dhahran, Jeddah, Doha, Dubai, Kuwait,
Manama, Muscat, Sanaa na Tripoli zinasema kuwa balozi zitasalia kufungwa hadi Jumamosi.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia iliongeza
kuwa balozi zake katika miji ya Antananarivo, Bujumbura, Djibouti,
Khartoum, Kigali na Port Louis pia zitafungwa . Idadi ya balozi za
Marekani zitakazofungwa kwa ujumla wiki hii ni 19.
Wizara hiyo ilisema kuwa uwezekano wa balozi hizo kushambuliwa ni kubwa sana hususan Mashariki ya kati na Afrika ya Kaskazini.
Hatua ya kufungwa kwa balozi hizo imekuja baada
ya kile Marekani kusema ilinasa ujumbe kutoka kwa kundi la wapiganaji wa
kiisilamu la al-Qaeda.
Inasemekana kuwa ujumbe huo ulikuwa kati ya viongozi wawili wakuu wa Al Qaeeda wakipanga mashambulizi.
Onyo hilo pia limetoa tahadhari kwa raia wa
Marekani kuwa waangalifu kuhusu tisho la makundi ya wapiganaji kufanya
mashambulizi dhidi ya mifumo ya usafiri wa umma pamoja na maeneo mengine
ya kitalii.
|
Habari hii kwa msaada wa BBC.
No comments:
Post a Comment