Katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi kwa Taifa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania amefafanua vizuri kuhusiana na habari zilizokuwepo kati ya mahusiano ya nchi yake na Nchi jilani ya Rwanda inayoongozwa na Rais Paul Kagame na haya ndo maneno ya Amirijeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Nchini Tanzania Mh,Jakaya Mrisho Kikwete "Ndugu wananchi;
Katika kipindi cha miezi miwili sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi
Mei, 2013, uhusiano baina ya nchi yetu na Rwanda unapitia katika wakati
mgumu. Kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yangu na nchi yetu ni ushahidi
wa kuwepo hali hiyo. Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na
ndugu zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa
Tanzania tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na
Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani. Kama majirani kila mmoja
anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano
mzuri.
Napenda kusisitiza kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa
mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yo yote
jirani au yo yote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni
mambo ambayo hayana tija wala maslahi kwetu.
Ndugu Wananchi;
Ukweli ni kwamba wakati wote tumekuwa tunajihusisha na mambo ya kukuza
na kujenga ujirani mwema na kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha
uhusiano wetu kwa maslahi ya nchi zetu. Hiyo ni moja ya nguzo kuu ya
Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu
na nchi ya Rwanda kabla na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa.
Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda kuwa kwa upande wetu
hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano
wetu. Mambo yapo vile vile. Kwa upande wangu, binafsi, sijasema lo lote
kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka
kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi
yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha. Sijafanya
hivyo kwa sababu sioni faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro
wa aina yo yote. Busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo.
Waingereza wanasema “two wrongs do not make a right”.
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo uhusiano wetu na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi.
Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa
na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika
Umoja wa Afrika na hata kimataifa. Uhusiano unaelekea kupata mtikisiko
baada ya mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na
mahasimu wao. Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado
naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia
hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali
ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Yoweri
Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema
cho chote pale mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza
kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.
Kwa kweli nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya. Havifanani kabisa, completely out of proportion and out of context.
Mimi nilifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za miaka mingi
katika ukanda wetu. Tumekuwa tunakutana katika mikutano na vikao
mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za
kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea. Wakati
wote tumeyachukulia kuwa ni mambo yanayotuhusu sote hivyo kupeana
ushauri ni wajibu wetu wote. Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana
kuzungumza tunautumia sana. Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane
jambo baya na la ajabu. Jambo la kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa
hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri si amri. Una hiyari ya
kuukubali au kuukataa. Muungwana hujibu: “Siuafiki ushauri wako”.
Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema
yasiyokuwepo na ya uongo.
Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia kusema kuwa mimi binafsi na Serikali yetu ya Tanzania
hatuna ugomvi wala nia yo yote mbaya na Rwanda. Tunapenda tuendelee
kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda. Labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi
yetu ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi tunasikia mengi
yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na
nchi yetu. Hatupendi kuyaamini moja kwa moja tunayoyasikia lakini
hatuyapuuzi." | |
No comments:
Post a Comment