Akaunti ya Twitter ya kundi la wanamgambo wa Al Shabaab imesitishwa kwa mara nyingine.
Ujumbe kutoka kwa Twitter katika akaunti yake ya
@HSMPress1 ulisema kuwa akaunti hiyo imefungwa, ingawa hapakuwa na
maelezo kwa nini hatua hiyo ilichukuliwa.
Katika taarifa iliyotumwa kwa
shirika la habari la AFP kundi hilo lililaani hatua ya Twitter na kusema
kuwa haitazaa matunda yoyote.
Mnamo siku ya Jumanne, Al Shabaab ilisema kuwa
ilishambulia msafara wa magari ya rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud,
ambaye hakujeruhiwa.
Hata hivyo habari hizo zilipuuzwa na ofisi yake
ikisema kuwa rais hakujeruhiwa kwani kifaa kililipuka mbali sana na
msafara wake.
Baadaye kundi hilo lilituma ujumbe kwa Twitter uliosema kuwa ,''Mara nyingine hautaponea ''kwa mujibu wa ripoti za , AFP.
Hata hivyo akaunti yake ya kiarabu ingali iko wazi.
Kwa mujibu wa sera ya Twitter, akaunti
zinazotumika kutuma vitisho,zinapaswa kufungwa. Akaunti pia zinaweza
kufungwa ikiwa zinatumiwa kwa shughuli zisizo halali.
Taarifa ya Al-Shabab ilisema kuwa haina akaunti
nyingine ya Twitter kwa kiingereza na kuwaonya watumiaji wa mtandao huo
kuwa wajiandae kwa akaunti zao kuvamiwa.
Akaunti ya Twitter ya kundi hilo kwa jina
@HSMPress, ilisitishwa mwezi Januari baada ya kundi hilo kuitumia kutuma
ujumbe wa kutisha kuwa lingewaua mateka wa Kenya na kisha kusema kuwa
limefanya hivyo.
Wadadisi wamesema kuwa katika siku za nyuma,
Marekani ililazimisha Twitter kufunga akaunti hiyo ingawa haikuwa na
nguvu za kisheria kufanya hivyo.
Hata hivyo Twitter inasema kuwa hakuna kitu
kinachoweza kuzuia Al Shabaab kuwa na akunti nyingine baada ya nyingine
za kwanza kufungwa.
Al-Shabab ilifungua akauti yake mara ya kwanza
mwezi Disemba mwaka 2011 baada ya wanajeshi wa Kenya , kwenda Somalia
kupambana na wanamgambo hao.
Wanamgambo hao wamefurushwa Mogadishu pamoja na kutoka miji mingine ingawa bado wanadhibiti sehemu nyingi za Kusini mwa Somalia.
|
No comments:
Post a Comment