Vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema, vimeungana kupinga mchakato wa
Katiba mpya kwa madai kuwa umehodhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
kutawaliwa na ubabe wa kanuni na sheria za Bunge kwa kuunyima upande wa
Zanzibar haki ya kushiriki.
Kutokana na hali hiyo, vyama hivyo ambavyo wabunge wake walitoka nje ya
ukumbi wa Bunge Septemba 4, 5 na 6, mwaka huu, vimetoa tamko la pamoja .
Akisoma tamko hilo lililosainiwa na wenyeviti wa vyama hivyo, Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema Katiba ya nchi ni mali ya
wananchi na sheria mama ya Taifa, hivyo mchakato wa mabadiliko yake
haupaswi kuhodhiwa na chama, taasisi, kundi au mtu yeyote.
“Mchakato wa Katiba mpya unapaswa kuwapa wananchi mfumo shirikishi na
utaratibu jumuishi wa kuwawezesha kuandika Katiba yao wakiongozwa na
misingi ya maridhiano,” alisema.
Alibainisha kuwa katika Mkutano wa 12 wa Bunge, Muswada wa Marekebisho
ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 ilipitishwa na
yaliyojiri kabla, wakati na baada ya kupitishwa yameweka mustakabali wa
mchakato shakani.
“Ikumbukwe kwamba kabla ya muswada huo kusomwa kwa mara ya pili, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ilitoa Rasimu ya Katiba ambayo ilijadiliwa na
makundi mbalimbali, kinyume na maoni hayo CCM imeweka msimamo wa kupinga
mambo makuu muhimu yaliyopendekezwa,” alisema na kuongeza kuwa imeweka
mikakati ya kukwamisha mabadiliko makubwa kuanzia katika Bunge Maalum la
Katiba.
Profesa Lipumba aliongeza kuwa Muswada huo umepitishwa ukiwa na
marekebisho yaliyomo kwenye muswada wenyewe na yaliyoongewa kupitia
jedwali la marekebisho yaliyowasilishwa na wabunge wa CCM.
“Hiyo inatoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na CCM kupitia Rais kuwa
na mamlaka makubwa zaidi katika uteuzi wa wajumbe 166 wa Bunge la
Katiba kutoka taasisi, asasi na makundi mbalimbali,” alisema.
Alisema marekebisho hayo yamefanyika kinyume na maoni ya wadau na
makubaliano ya awali ya kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala
baada ya kupokea maoni ya wadau wa Tanzania Bara na kamati haikukutana
kabisa na wadau wala Wawakilishi wa wananchi wa upande wa Zanzibar.
Alisema Zanzibar haikushirikishwa kikamilifu katika kuandaa muswada huo
na Mei, mwaka huu, serikali ya Muungano ilipeleka Muswada wa Mabadiliko
ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliokuwa na vifungu sita na Zanzibar
waliujadili na kupeleka mapendekezo ya rasimu ya muswada huo.
“Muswada uliopelekwa Bungeni uliongezewa vifungu vingi ambavyo havikuwamo katika rasimu iliyopelekwa Zanzibar,” alisema.
Profesa Lipumba alisema kifungu cha 26 cha sheria mama kurekebishwa
kuruhusu iwapo theluthi mbili za kila upande hazitapatikana kwa mara
mbili, basi kura kwa mara ya tatu itakuwa kwa wingi wa kawaida ya kila
upande.
Alisema kifungu cha 37 kinachoruhusu kuvunjwa kwa Tume ya Katiba
kimerekebishwa bila mashauriano katika Bunge la Katiba na siyo kama SMZ
ilivyoafiki awali kuwa Tume itavunjwa baada ya matokeo ya kura ya maoni.
“Yaliyojiri Bungeni na yanayoendelea kusemwa na kutendwa na CCM na
serikali juu ya muswada huo ni matokeo ya mikakati, hivyo nguvu za
pamoja za wananchi, wadau na wenye kuitakia mema nchi yetu zinapaswa
kuunganishwa.
MAAZIMIO YA VYAMA.
Alisema vyama hivyo vimedhamiria kuunganisha umma kufanya maamuzi ya
kunusuru mchakato huo kuendelea kutekwa na kuhodhiwa na CCM kwa
kuzingatia kwamba madaraka na mamlaka yote ya wananchi na serikali
inapaswa kuwajibika kwa wananchi.
Aidha, alisema Septemba 21, mwaka huu, watafanya mkutano wa hadhara
uwanja wa Jagwani jijini Dar es Salaam, ambao utakuwa mwanzo wa hatua za
kwenda kwa wananchi ili kuwaunganisha kuchukua hatua.
Alisema mikutano hiyo itakuwa endelevu kwa maeneo mengine nchini kwa
viongozi wa vyama hivyo kuzungumza na Watanzania ili kuungana pamoja
kupinga mchakato kuhodhiwa.
Pia, vinawapongeza na kuwaunga mkono wabunge wa vyama vyao walioweka
pembeni tofauti zao za kivyama na kutumia njia za kibunge kutaka mjadala
wa muswada huo usiendelee bungeni kwa lengo la kuhakikisha masuala
muhimu kwa niaba ya wananchi yanazingatiwa.
KAULI YA MBOWE
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema vyama hivyo vinaziomba
asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, taasisi za
elimu ya juu, vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji,
wavuvi, taasisi za sekta binafsi, watu wenye ulemavu, wataalam wa
masuala mbalimbali, wanawake, vijana, vyama vya wastaafu na makundi
mengine, kuweka kando tofauti zao na kujikita kwenye mchakato huo.
Aidha, alivitaka vyombo vya habari kuunga mkono na kwamba muungano huo
uko tayari kushirikiana na wana-CCM na viongozi wa serikali wenye
mapenzi mema na Tanzania kwa miaka 50 au 100 ijayo.
Alisema tatizo kubwa ni baadhi ya viongozi kufanya mchakato wa Katiba
kama suala la kizazi cha sasa na kusahau suala hilo ni la vizazi vijavyo
na Katiba ni ya Watanzania wote na si chama au viongozi.
“Mkataba wa Katiba ndiyo sehemu pekee ya Watanzania kutibu majeraha
waliyonayo, CCM inapoteza mwelekeo wanatumia ubabe, kanuni na wingi wao
ndani ya Bunge kuburuza mchakato wa Katiba,” alisema.
Alisema viongozi wanahubiri amani, lakini wanayotenda hayaendani na
kutaka amani ya Tanzania idumu kwani licha ya kuwapo viashiria vya
kutoweka kwa amani, mchakato wa Katiba unalazimishwa kuongezwa kama
kiashiria kingine.
MBATIA ANENA
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema vyama hivyo vinamuomba
Rais Jakaya Kikwete, kutosaini muswada huo kwa kuwa hautasaidia
upatikanaji wa Katiba yenye ushirikishwaji wa wananchi.
“Tunamtahadharisha Rais Kikwete, historia isije ikamhukumu kwa kusaini
muswada huo ambao umepitishwa kinyemela, aweke maslahi ya Taifa mbele na
si chama chake ambacho ni Mwenyekiti wa Taifa…mkono wake usitumbukize
Taifa kwenye machafuko,” alisema.
Aidha, vyama hivyo vimesema havitakwenda Ikulu kwa ajili ya kuonana na
Rais ila zaidi vitaelekeza nguvu kwa wananchi wenye Katiba yao na
kumsihi Rais kutosaini muswada huo kwa kuwa mkono wake ndiyo unasubiriwa
kuamua hatma ya Taifa kwa miaka mingi ijayo.
Septemba 6, mwaka huu, wakati wa kikao cha Bunge palitokea purukushani
kubwa kiasi cha wabunge na askari wa Bunge kutwangana makonde hadharani,
baada ya Naibu Spika, Job Ndugai, kukataa kumruhusu Mbowe kama Kiongozi
Rasmi wa Kambi ya Upinzani kutoa hoja aliyokuwa nayo.
|
No comments:
Post a Comment