Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema
kitamshitaki Balozi wa China nchini, Lu Younqing Umoja wa Mataifa (UN)
kwa kukiuka Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa mwaka 1964 ambao
unaeleza uhusiano wa kibalozi kati ya nchi na nchi.
Aidha, kimesema kitaiandikia barua Serikali ya
China ili kutaka ufafanuzi kama imemtuma Balozi wake kufanya kazi ya
uenezi siasa kwenye vyama.
Tukio la Balozi huyo kuhudhuria mkutano wa hadhara
wa CCM lilitokea Septemba tisa mwaka huu kwenye mkutano wa chama hicho
uliofanyika Wilaya ya Kishapu Shinyanga, ambapo Katibu Mkuu wake,
Abdulrahman Kinana alimtambushisha balozi huyo huku akiwa amevaa sare za
chama hicho.
Waziri kivuli wa mambo ya nje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana
Jijini Mwanza, Ezekiel Wenje alisema Chadema wameamua kuchukua hatua
hizo ili kukomesha vyama vya siasa kutumia mabalozi kama wawakilishi wa
vyama vyao kwa kufanya uenezi kwenye mikutano ya siasa.
Kwa upande wa Katibu Mkuu Taifa wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema chama chake kinaangalia namna ya
kumchukulia hatua za kumshtaki Balozi huyo akidai kuwa kitendo cha
kushiriki siasa za CCM na kisha kuvalishwa kofia ya chama hicho ni
kiunyume na taratibu za UN.
“Mkataba wa Vienna Convention wa mwaka 1964 Ibara ya 41 kifungu kidogo
cha kwanza kinakataza mabalozi kujiingiza kwenye mambo ya ndani ya nchi
ikiwa pamoja na kufanya siasa.
Kwa upande wa Waziri wa nchi za nje na ushilikiano wa kimataifa Bernard Membe amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa kitendo kilichofanywa na Balozi huyo siyo sahihi na kinakiuka mkataba wa Vienna.
“Wizara inapenda kutamka kwamba kitendo cha Balozi yoyote kuhudhuria
mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya
vyama vya siasa siyo sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba
wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia,” alisema
Membe katika taarifa yake jana jioni.
Taarifa hiyo ilisema kuwa mkataba huo unazuia wawakilishi wa nchi za nje
kujihusisha na ushabiki wa kisiasa wanapofanya kazi zao kwenye nchi za
uwakilishi.
“Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012, Wizara ilikumbana na vitendo
vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki, kadhalika kwa
tukio hili Wizara itachukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili
kuzuia jambo hili lisitokee tena,” alisisitiza.
Taarifa hiyo ilisema kuwa Balozi huyo alikwenda wilayani humo kuhudhuria
uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba vinavyojengwa na
mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo vitakuwa na
uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika
mwakani.
Alisema Wizara imeona picha na habari kwenye vyombo vya habari zikieleza na kumuonyesha Balozi huyo akiwa kwenye mkutano wa CCM.
No comments:
Post a Comment