Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametengua maamuzi yaliyofanywa na Waziri wa
Ujenzi Dk. John Magufuli ya kuongeza tozo ya asilimia tano kwa
wasafirishaji wa malori na mabasi kwa uzito unaozidi.
Agizo la kurudisha asilimia hiyo ya tozo ilitangazwa na Dk. Magufuri
Oktoba Mosi mwaka huu na kusababisha manung’uniko kutoka kwa
wasafirishaji huku wa malori wakigoma kuanzia juzi.
Waziri Mkuu aliitangaza uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari.
Pinda alisema baada ya kukutana na wadau wa usafirishaji nchini na
kusikiliza maelezo yao, alibaini masuala kadhaa ambayo aliona ni vyema
yakaangaliwa upya ili sekta hiyo isizorote na baada ya hapo alikutana na
Baraza la Mawaziri na kukubaliana mambo kadhaa.
“Kwa kuwa kuna mvutano kati ya Wizara ya Ujenzi na wasafirishaji wa
malori na mabasi kuhusu kanuni ya 7 (3) ya Sheria ya Usafirishaji ya
mwaka 1973, kwamba haitekelezeki kirahisi, nimeiagiza wizara ikutane
na wadau mbalimbali kwa ajili ya kupitia kila jambo linalohitajika,”
alisema.
Wadau hao ni Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Viwanda na
Biashara, Chama Cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Chama cha Wamiliki wa
Malori (Tatoa), Ofisi ya Waziri Mkuu na ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG).
Pinda alisema: “Tumewapa mwezi mmoja wa kulishughulikia suala hili kwani
ni jambo linalohitaji uamuzi mzuri, na tunategemea kuwa watakuja na
majibu mazuri kwa muda tuliowapa.”
Aliongeza: “Nalisema hili kwa kuwa sisi kama nchi tunapaswa kuliangalia
vizuri, na ni lazima tuziangalie barabara zetu tunazozijenga kwa gharama
kubwa.”
Pinda alisema kutakuwa na uwezekano wa kuwapo kwa msongamano wa mabasi
na malori kwenye mizani na serikali imeshauri kuwa mizani ya Kibaha
itumike kwa ajili ya mabasi tu na ile ya Mikese kwa ajili ya malori, na
kwamba njia za Tanga, Moshi na Arusha zitalazimika kutafutiwa utaratibu
mwingine wa mizani.
Pia aliitaka timu hiyo, wakati wa majadiliano yao, kuangalia suala la watumishi ambao siyo waaminifu kwenye mizani.
“Wakati naongea na wadau hao mmoja aliniambia kuwa bado kuna matatizo
kwenye mizani kwani alisema gari lake lilizuiliwa kwa kuwa lilipatikana
na kosa, lakini alitoa rushwa na akaachiwa, kwa hiyo tatizo hilo bado
lipo na linapaswa kuangaliwa,” alisisitiza.
Alisema jambo jingine linalopaswa kuangaliwa ni hali ya mizani, kwani
kuna malalamiko kuhusu utofauti wa uzito katika baadhi ya mizani na
kwamba amehakikishiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kwamba
wapo mbioni kufunga mizani nyingine ambazo ni za kisasa zaidi.
Pia alitaka kuwapo kwa mawasiliano kati ya taasisi za serikali hasa pale
linapotokea jambo linaloigusa sekta nyingine ili wapate kuzungumza na
kwamba katika hali ya sasa ni vyema ukawapo utaratibu wa kuwashirikisha
wadau katika kila sekta hizo ili kuleta uelewano.
Kuhusu chimbuko la mgogoro, Pinda alisema kulikuwa na mambo mawili,
ambayo ni barua ya aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wa wakati huo, Basil
Mramba, ambayo aliiandika mwaka 2006 ya kutoa msamaha kwa tozo kwa uzito
wa magari uliozidi ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubaliwa
kisheria.
“2006 Mramba alipata taarifa kuwa mizani ina matatizo na akaona aweke
utaratibu wa ahueni kidogo, kwa hiyo barua hiyo ikawa inatumika isivyo
sawa kwani kila aliyezidisha uzito alitumia mwanya huo ili asilipishwe
na hivyo kuchangia kutokuwapo kwa uadilifu,” alisema.
Alitaja jambo lingine kuwa ni la kisheria, na kwamba Waziri Magufuli
aliamua kutumia sheria kwa kuwa mwongozo wa Mramba haukuwa wa kisheria
pamoja na kwamba uamuzi wake ulikuwa na nia njema.
|
No comments:
Post a Comment