Mahakama ya kimataifa ya ICC, imetoa kibali cha
kukamatwa kwa raia Mkenya ambaye anatuhumiwa kwa kujaribu kuwahonga
mashahidi ili wajiondoe kwenye kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya William
Ruto.
Viongozi wa mashtaka walisema kuwa mshukiwa huyo
Walter Osapiri Barasa(Pichani) ameshtakiwa kwa makosa matatu ikiwemo kutumia
njia za ufisadi kumshawishi shahidi mmoja na mkewe kwa kumlipa shilingi
milioni 1.4 au dola 16,200, ili wajiondoe kama mashahidi katika kesi
hiyo.
Aidha mahakama inasema kuwa ni juu ya Kenya sasa kumkamata Barasa.
Kiongozi wa mashtaka Fatou Bensouda amesema kuwa
ana ushahidi wa kutosha kuonyesha njama ya Barasa kutaka kuwahonga
mashahidi ili wajiondoe katika kesi dhidi ya Ruto.
Bensouda amesema kuwa kuna mtandao wa watu wanaofanya kila wawezalo ili kuporomosha kesi dhidi ya Ruto.
Lakini Barasa amesema kuwa yuko tayari kujitetea mbele ya mahakama hiyo na kuonyesha kuwa hana hatia.
Naibu Rais Ruto na Rais Kenyatta wameshtakiwa
kwa kupanga na kuongoza ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo
watu 1,200 walifariki.
|
No comments:
Post a Comment