Friday, August 23, 2013

HIVI NDIVYO RUBANI WA NDEGE HII ALIVYOWEZA KUOKOA MAISHA YA ABIRIA WAKE.

Abiria sita na rubani wamenusurika kufa baada ya ndege ndogo aina ya Vich Grave waliyokuwa wakiruka nayo kupata dharura na kuanguka katika Ziwa Manyara.

Imelezwa kuwa ndege hiyo yenye namba za usajili 5H /EPW mali ya TanzaAir ilipata hitilafu katika injini yake moja hatua ambao ilimlazimu rubani wake aliyetambulika kwa jina moja la Kapteni Kondo
(51) kuishusha lakini ikaanguka kwenye ziwa hilo.

Abiria hao walipata majeraha madogo madogo na kukimbizwa hadi Hospitali ya Selian inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Kati jijini hapa kwa matibabu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema ndege hiyo ilikuwa ikitokea Bukoba kwenda jijini Dar es Salaam kupitia Zanzibar.

Aliwataja abiria hao kuwa ni Anik Kashasa (51), Regina Mtabihirwa(58), Aloyce Mwanga (60), Naburi Meeda (80), Ashura Mohamed (38)pamoja na Protas Ishengoma (45) wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Alisema abiria hao waliokolewa kwa kutumia mitumbwi ya wavuvi na kisha walichukuliwa na chopa hadi Arusha kwa matibabu.

Alisema ilianza safari yake juzi majira ya saa 12:58 asubuhi na hitilafu hiyo ilitokea majira ya saa 2:43 jana asubuhi eneo la Iambi Kusini, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara.

Kamanda Sabas ambaye alikuwepo eneo la tukio, alisema ndege hiyo ilipofika hapo maeneo hayo, rubani aligundua kuwa ina hitilafu na kwamba asingeweza kuendelea na safari ili aweze kutua Uwanja wa Ndege
wa Arusha, hivyo alazimika kuiangushia ziwani ili kunusuru maisha ya abiria.

Alisema ndege hiyo imeharibika lakini ripoti kamili itatolewa baada ya kufika kwa wataalam na kufanya uchunguzi wa chanzo chake.

Tukio la kuanguka kwa ndege hiyo ni la tatu kutokea mwaka huu katika mikoa ya Arusha na Manyara ambapo tukio la kwanza ni la mfanyabiashara maarufu Babu Sambeki alianguka Aprili mwaka huu na ndege yake wakati alipojaribu kutua katika Uwanja wa Ndege wa Arusha ambapo alifariki papo hapo.

Ndege hiyo ilianguka baada ya kuparamia jirani na uwanja huo.Tukio lingine ni la ndege ya madaktari  inayomilikiwa na Kanisa katoliki , kuanguka na kujeruhi vibaya abiria saba wakiwemo rubani wawili muda mfupi baada ya kuruka katika kiwanja kidogo cha ndege katika kijiji cha  Merugwayi, wilayani Longido mkoani Arusha.

  Kwa niaba ya wasomaji wa blog hii atuna budi kumpongeza rubani huyo kwa ujasili aliouonyesha na kutumia weledi wa kazi yake kuokoa maisha ya watu waliokuwemo katika Ndege hiyo.

                                                   


 ...

No comments:

Post a Comment