Thursday, August 15, 2013

NECTA KUANZA KUTUMIA KUSAHIHISHA MITIHANI YA KUJIELEZA KWA KOMPYUTA

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Joyce Ndalichako(Pichani) amesema baraza lake linajiandaa kutumia teknolojia ya kompyuta wakati wa kusahihisha maswali ya mitihani ambayo wanafunzi wanajibu kwa kujieleza.

Kwa sasa teknolojia ya usahihishaji kwa kompyuta inayotumika nchini ni ile ya kujibu maswali ya kuchagua tu ya`Optical Mark Reader’ (OMR) iliyoanza kutumika mwaka jana kusahihisha mitihani ya darasa la saba.

Akizungumza katika Mkutano wa Mabaraza ya Mitihani Afrika (AEAA), unaoendelea mkoani Arusha, Dk Ndalichako alisema: “Kwa kuanzia, Necta itafanya majaribio ya teknolojia hiyo mwakani na ninaamini itaongeza ubora katika usahihishaji.”

“Kwa kutumia hii teknolojia msahihishaji hawezi kuona namba ya mwanafunzi, anachoona ni sehemu ya swali anayotakiwa kusahihisha na jibu lake, akimaliza swali moja jingine linakuja moja kwa moja,”.

Alisema kwa kutumia teknolojia hiyo, mratibu wa usahihishaji anaweza kuona kazi inayofanywa na msahihishaji yeyote na hata kuwapima kama atakuwa na wasiwasi wowote.

Alisema Zimbabwe imeanza kutumia teknolojia hiyo aliyosema itasaidia kuongeza ubora katika suala la usahihishaji.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo aliendelea kusema teknolojia ya OMR imeongeza ubora wa hali ya juu kwenye mtihani wa darasa la saba pamoja na usahihishaji wake.

“Watu wanasema kuwa mtihani wa maswali ya kuchagua ni mrahisi, lakini hii siyo kweli, inatungwa na wataalamu na inalenga kumpima mtoto katika kila nyanja, ndiyo maana hata mtihani wa darasa la saba mwaka jana ilibidi Serikali ishushe alama za kwenda kidato cha kwanza zikawa 70 badala ya 100,” alisema Dk Ndalichako.

Akizungumzia teknolojia hiyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema wamebaini kuwa zaidi ya asilimia 80 ya nchi za Afrika zinatumia mfumo wa usahihishaji kwa OMR.

Alisema baadhi ya nchi zimeanza kusahihisha kwa kutumia kompyuta hata katika maswali ya kujieleza na kuwataka Watanzania kuacha kujirudisha nyuma.


No comments:

Post a Comment