Monday, August 5, 2013

WABUNGE WA VITI MAALUM HAWANA UMUHIMU SITTA AFUNGUKA TENA.

Spika wa zamani wa Bunge la Tanzania Samuel Sitta ambae kwa sasa ni Waziri wa Afrika mashariki amenukuliwa akisema“Ninakerwa sana na mfumo wa Viti Maalumu, kwanza sioni umuhimu wa mfumo huu kuendelea kuwepo katika Katiba Mpya. Hawana umuhimu wowote.”

Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Nyamikoma, Kata ya Busega Mkoa wa Simiyu Julai 29, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuimarisha uhai wa chama, Sitta aliwajia juu bila ya kuwataja baadhi ya wabunge wa CCM.

“Wanakwenda bungeni hawachangii, hawana hata hoja za kuchachafya upinzani, hawachangii, hawa ni mzigo,” alisema Sitta na kuongeza: “Wapo baadhi ya wabunge, hawajawahi hata siku moja kwenda kwenye majimbo yao kuwatembelea wananchi waliowachagua... Inawezekana hata wapiga kura wakawa wamewasahau. Hawa hawafai hata kuchaguliwa wakiomba tena kura.”

“Rais Jakaya Kikwete amejitahidi sana kuleta mabadiliko, ameleta mafanikio ya uchumi na mambo mengi. Inatakiwa wabunge waende wakawaeleze wananchi maendeleo haya, inawezekana hawayajui lakini watu hawaendi jimboni, wananchi watayafahamu vipi haya maendeleo?”

Juzi, akizungumzia wabunge wa Viti Maalumu, Sitta alisema... “Wengi wao hawachangii chochote na mbaya zaidi hakuna wa kuwahoji chochote kama wabunge wanavyorudi jimboni.

“Ikifika wakati wa posho wapo. Sisemi kama naumia wao kuchukua posho.... hawa wanachukua posho wanawajibika kwa nani? Nani anahoji utendaji wao na zaidi itakapokuja Katiba Mpya ya kuwawajibisha wabunge wazembe, hawa watawajibishwa wapi?”

“Rasimu ya Katiba Mpya isiwaruhusu hawa... hawa nao ni mzigo mwingine. Wakifika bungeni hawachangii chochote, hawawezi kuwajibishwa na yeyote kwa mfumo uliopo na pia hawawajibiki popote, sasa huu si mzigo?”Ikumbukwe pia mke wake ni Mbunge wa viti maalum.


No comments:

Post a Comment