Wednesday, October 2, 2013

MAHAKAMA YA KIMATAIFA (ICC) YATOA KIBALI CHA KUKAMATWA ANAEDAIWA KUTAKA KUHONGA MASHAIDI.

Mahakama ya kimataifa ya ICC, imetoa kibali cha kukamatwa kwa raia Mkenya ambaye anatuhumiwa kwa kujaribu kuwahonga mashahidi ili wajiondoe kwenye kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya William Ruto.

Viongozi wa mashtaka walisema kuwa mshukiwa huyo Walter Osapiri Barasa(Pichani) ameshtakiwa kwa makosa matatu ikiwemo kutumia njia za ufisadi kumshawishi shahidi mmoja na mkewe kwa kumlipa shilingi milioni 1.4 au dola 16,200, ili wajiondoe kama mashahidi katika kesi hiyo.

Aidha mahakama inasema kuwa ni juu ya Kenya sasa kumkamata Barasa.

Kiongozi wa mashtaka Fatou Bensouda amesema kuwa ana ushahidi wa kutosha kuonyesha njama ya Barasa kutaka kuwahonga mashahidi ili wajiondoe katika kesi dhidi ya Ruto.

Bensouda amesema kuwa kuna mtandao wa watu wanaofanya kila wawezalo ili kuporomosha kesi dhidi ya Ruto.

Lakini Barasa amesema kuwa yuko tayari kujitetea mbele ya mahakama hiyo na kuonyesha kuwa hana hatia.

Naibu Rais Ruto na Rais Kenyatta wameshtakiwa kwa kupanga na kuongoza ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo watu 1,200 walifariki.

Habari hii kwa hisani ya BBC.

No comments:

Post a Comment