Thursday, July 25, 2013

SAMUEL SITA AFUNGUKA NCHI KUWA NA MARAIS WA TATU NI WIZI MTUPU.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta  na Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, amesema litakuwa jambo la kuchekesha duniani iwapo nchi maskini kama Tanzania itakuwa na marais watatu kama muundo wa serikali tatu uliopendekezwa kwenye rasimu ya katiba mpya utapitishwa.

Vile vile, amesema licha ya kuwa kichekesho, muundo wa muungano ambao utatengeneza marais watatu utasababisha gharama kubwa za uendeshaji na kuwa mzigo mkubwa kwa uchumi. Aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa Baraza la Taifa la Vijana la Rasimu ya Katiba mpya unaoendelea jijini Dar es Salaam.

Alisema inawezekana kabisa Tanzania ikawa na serikali tatu lakini wakati huo huo ikawa na rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wengine wakapewa majina mengine kama Makamu wa Rais ama Waziri Mkuu.

Sitta alisema kimsingi hapingi muundo wa serikali tatu bali anachopinga ni utitiri wa marais unaoweza kutokea ambao utasababisha gharama kubwa za uendeshaji wa serikali.

“Hebu fikiria tunakuwa na marais watatu, Rais wa Zanzibar anasafiri kwenda nje, Rais wa Jamhuri ya Muungano naye anasafiri, Rais wa Tanganyika naye anakwenda nje ya nchi, hivi huko nje si watatushangaa na kutuona kioja jamani nchi maskini inafanya hivi,” alisema.

Aidha, Sitta alisema inawezekana kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale watakaoongoza Zanzibar na Tanganyika wakapewa nafasi kama za Makamu wa Rais, Naibu Rais ama Waziri Mkuu.

Sitta alisema watu wanaopigia debe utitiri wa marais ni wale wenye uroho wa madaraka ambao wanadhani inaweza kuwa njia rahisi kwao kufikia malengo yao ya kisiasa.

“Mimi nadhani huu ni ubinafsi wa hali ya juu, kila mtu nchi hii anataka kuitwa mheshimiwa rais, mimi nashauri kama muundo wa serikali tatu utapitishwa basi tuwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hao wengine watafutiwe majina mengine,” alisema Sitta.

Aliendelea kusema kuwa Watanzania wanapaswa kusimama kidete kuhakikisha Katiba ijayo haitengenezi rais wala serikali dikteta ili nchi iende kwa misingi ya demokrasia na utawala bora.

Alisema Katiba mpya lazima iweke misingi ambayo itawaongoza viongozi watakaochaguliwa kuacha ubinafsi wa kujali familia zao badala ya maslahi ya umma.

“Tuwe na Katiba ambayo kiongozi akikabidhiwa madaraka anajua kabisa kwamba hapa niko kwa ajili ya kuangalia maslahi ya umma, kuna viongozi badala ya kuhangaika na masuala yanayohusu wananchi wanahangaika na maslahi binafsi na familia zao,” alisema.

Alisema Katiba iwe na vipengele vya kuhakikisha nchi inakuwa na misingi ya utawala bora itakayowabana viongozi waroho kutumia madaraka yao vibaya na kwa maslahi yao.

Alisema hatari anayoiona sasa ni kwa baadhi ya viongozi kuhangaika kuingiza mambo binafsi yenye maslahi yao ndani ya Katiba badala ya kuangalia utaifa.

“Tukiacha hali hii iendelee na hawa watu wakachomeka chomeka mambo yao binafsi mwisho wa siku Katiba hii hii itakuwa chungu kwetu…hata hii mivutano inayoendelea ya tuwe na marais wangapi kuna watu wanataka kuingiza maslahi yao hapa,” alisema.

Sitta alisema Katiba mpya lazima ipunguze gharama za uendeshaji na kuongeza kuwa hata Mawaziri 15 waliopendekezwa kwenye serikali ya Muungano ni wengi kuliko mahitaji yenyewe.

Alisema mataifa mengi ya Afrika yanatumia fedha nyingi katika uendeshaji wa serikali wakati wananchi wakiteseka kwenye lindi la umaskini.

“Kama kuna masuala saba tu yanayohusu Muungano, hao mawaziri 15 wote wanini? Wabunge 150 wote wa kazi gani kama si kufuja uchumi wa nchi, mimi naona hizi ni mbwembwe ambazo hazina maana sana kwa maendeleo ya watu,” alisema. 

KIFUNGU KATIKA RASIMU MPYA YA KATIBA KINASEMA

57.-(1) Jamhuri ya Muungano itakuwa na muundo wa shirikisho lenye
serikali tatu ambazo ni:
(a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(b) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; na
(c) Serikali ya Tanzania Bara.
(2) Shughuli za Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kusimamiwa
na:
(a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
(b) Bunge la Jamhuri ya Muungano; na
(c) Mahakama ya Jamhuri ya Muungano.
(3) Muundo, madaraka na mambo mengine ya kiutendaji yahusuyo
Serikali yaTanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yataainishwakatika Katiba za Washirika wa Muungano.Zaidi ukiwa Mtazania itafute uisome na utoe maoni yako kwa mustakabari wa taifa lako na vizazi vijavyo.


No comments:

Post a Comment