Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemfungulia mashtaka
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutokana na kauli yake aliyoitoa bungeni hivi
karibuni kwamba wanaokaidi maagizo ya dola wapigwe.
Hatua hiyo ya LHRC imepingwa vikali na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma
(DPP), Dk Elieza Feleshi akisema hakuna uhalali wa mashtaka yoyote dhidi
ya kiongozi huyo sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni haikuwa piga ua.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo Bisimba alifungua mashtaka hayo
katika Mahakama Kuu akisema kuwa wanamshtaki Waziri Mkuu kwa
maelezo kuwa amekiuka kifungu cha Katiba Ibara 13 (1). Pinda ametajwa
kuwa ni mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 24.
Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa LHRC, Harold Sungusia alisema
kwamba, mwingine aliyeunganishwa katika kesi hiyo ya kikatiba
iliyofunguliwa na LHRC na Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Alisema katika kesi hiyo, kuna jopo la mawakili wasiopungua 20 na kwamba
wamepata saini za wananchi 2,029 wanaopinga kauli hiyo ya Pinda na
kuunga mkono kufunguliwa kwa kesi hiyo.
Mjumbe wa Bodi ya LHRC, Wakili Dk Ringo Tenga alisema katika kesi hiyo
wameangalia zaidi sheria na hasa haki za msingi za binadamu na kwamba
kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda inahatarisha haki hizo.
Kauli yenyewe
Wakati wa Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu bungeni,
Juni 19, mwaka huu, Waziri Mkuu akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari
kiasi gani kubainisha na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusakama
makundi fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na
jinsi gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko
katika baadhi ya maeneo kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo
vya dola?”
Waziri Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema... mwishowe unaona anasema
vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki,
ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna nyingine, maana wote
tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe
ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu
hakuna namna nyingine... maana tumechoka.” Kesi hiyo itakayosikilizwa na
majaji watatu, haina uhusiano na kesi nyingine ambazo wajibu maombi
hupewa siku 90 kujibu hoja zilizowasilishwa. Kesi hiyo imefunguliwa kwa
mujibu wa Katiba Sura ya Tatu.
Akizungumza juzi kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma baada ya kufungwa
kwa Warsha ya Wapelelezi na Waendesha Mashtaka wa Serikali ngazi ya
mikoa, Dk Feleshi alisema hakuna uhalali wa mashtaka hayo kwa sababu
kauli ya Pinda kuwa pigeni haikuwa piga ua.
“Hii haikuwa kuchochea apige watu, alichosema ni kupiga wale wasiotaka
kutekeleza amri halali na zaidi alisema piga lakini si kupiga na kuua,”
alisema.
Mkutano huo uliendeshwa chini ya ulinzi mkali huku kukiwa na udhibiti wa
kuvuja siri kwa kiwango cha juu. Pamoja na mambo mengine, ulikuwa
ukijadili mbinu za kisasa katika kuendesha kesi pamoja na kujiuliza
sababu za Serikali kushindwa katika kesi nyingi.
“Kwa sababu lile neno kupiga ni lazima lipewe maana pana huwezi kumpiga
tu mtu hivihivi ambaye hakuvunja sheria lakini nilivyoelewa, ilikuwa ni
hivyo, ni sawa na mtu ambaye anamshambulia askari,” alisema Dk Feleshi.
Alisema kuna sheria ya kutumia nguvu pale ambako kuna mkusanyiko
usiokuwa wa halali pindi raia wanapokaidi kutawanyika kwa hiari hivyo
hakuna shaka kauli ya Waziri Mkuu ililenga hivyo.
Hata hivyo, alisema hajapata taarifa za LHRC kumshtaki Waziri Mkuu
kimaandishi na kwamba akizipata atatoa ufafanuzi baada ya kuona lengo la
mashtaka.
Msimamo
Akizungumza baada ya kufungua mashtaka hayo, Dk Bisimba alisema Waziri
Mkuu anaweza kushtakiwa kwa kuwa alizungumza kwa nafasi yake ya Waziri
Mkuu na si mbunge na kusisitiza kwamba hakuna aliye juu ya sheria na
kudai kwamba kauli hiyo ni kinyume cha Katiba.
Alisema kuwa kila anayevunja Katiba lazima ashughulikiwe kisheria na
kwamba mahali pake ni mahakamani tu. Alisema kwa mujibu wa hati hiyo ya
madai, kauli na amri kama hizo zinapotolewa na kiongozi mwenye hadhi
kama ya mdaiwa wa kwanza (Waziri Mkuu) huchukuliwa kama sheria
inayopaswa kutekelezwa na wakala wa utekelezaji wa sheria kama vile
polisi. Wadai hao wanadai kuwa kwa ufahamu wao polisi wanaweza
kuchukulia kauli hiyo kama amri halali kutoka kwa mkubwa wao na hivyo
kuwapiga na kuwatesa watu wasio na hatia, kinyume cha Katiba.
Pia wanadai wanatambua kuwa Ibara ya 100 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inatoa kinga kwa wabunge na uhuru wa maoni bungeni.
Hata hivyo, wanatambua kuwa Ibara ya 100 (2) ya Katiba hiyo
inawawajibisha wabunge wote chini ya masharti ya Katiba na kwamba kauli
aliyoitoa Waziri Mkuu Pinda inakiuka Ibara ya 12(12).
Hivyo wanaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa kauli na amri hiyo aliyoitoa Pinda inavunja Katiba.
Mkurugenzi wa taasisi inayofuatilia Mwenendo wa Bunge (Watch), Marcos
Albania alidai kwamba wamegundua kuwa kauli hiyo ya Pinda ni moja kati
ya matamko makubwa yanayovunja Katiba.
Alisema mbali na shtaka hilo, kuna la pili dhidi ya Waziri Mkuu Pinda,
ambalo hawajalifikisha mahakamani ambalo pia linatokana na kauli hiyo
aliyoitoa bungeni kwamba: “Sasa wamechoka".hapo chini ni video ya kauli ya Waziri mkuu alipokuwa akielezea unaweza kuitazama pia....
.....>>>.
|
No comments:
Post a Comment