Monday, September 16, 2013

MUUNGANO HUU UTAMSHAWISHI RAIS ASITISHE KUTIA SAINI MUSWADA WA KATIBA ILI UWE SHERIA?

Vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema, vimeungana kupinga mchakato wa Katiba mpya kwa madai kuwa umehodhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutawaliwa na ubabe wa kanuni na sheria za Bunge kwa kuunyima upande wa Zanzibar haki ya kushiriki.

Kutokana na hali hiyo, vyama hivyo ambavyo wabunge wake walitoka nje ya ukumbi wa Bunge Septemba 4, 5 na 6, mwaka huu, vimetoa tamko la pamoja .

Akisoma tamko hilo lililosainiwa na wenyeviti wa vyama hivyo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema Katiba ya nchi ni mali ya wananchi na sheria mama ya Taifa, hivyo mchakato wa mabadiliko yake haupaswi kuhodhiwa na chama, taasisi, kundi au mtu yeyote.

“Mchakato wa Katiba mpya unapaswa kuwapa wananchi mfumo shirikishi na utaratibu jumuishi wa kuwawezesha kuandika Katiba yao wakiongozwa na misingi ya maridhiano,” alisema.

Alibainisha kuwa katika Mkutano wa 12 wa Bunge, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 ilipitishwa na yaliyojiri kabla, wakati na baada ya kupitishwa yameweka mustakabali wa mchakato shakani.

“Ikumbukwe kwamba kabla ya muswada huo kusomwa kwa mara ya pili, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa Rasimu ya Katiba ambayo ilijadiliwa na makundi mbalimbali, kinyume na maoni hayo CCM imeweka msimamo wa kupinga mambo makuu muhimu yaliyopendekezwa,” alisema na kuongeza kuwa imeweka mikakati ya kukwamisha mabadiliko makubwa kuanzia katika Bunge Maalum la Katiba.

Profesa Lipumba aliongeza kuwa Muswada huo umepitishwa ukiwa na marekebisho yaliyomo kwenye muswada wenyewe na yaliyoongewa kupitia jedwali la marekebisho yaliyowasilishwa na wabunge wa CCM.

“Hiyo inatoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na CCM kupitia Rais kuwa na mamlaka makubwa zaidi katika uteuzi  wa wajumbe 166 wa Bunge la Katiba kutoka taasisi, asasi na makundi mbalimbali,” alisema.

Alisema marekebisho hayo yamefanyika kinyume na maoni ya wadau na makubaliano ya awali ya kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala baada ya kupokea maoni ya wadau wa Tanzania Bara na kamati haikukutana kabisa na wadau wala Wawakilishi wa wananchi wa upande wa Zanzibar.

Alisema Zanzibar haikushirikishwa kikamilifu katika kuandaa muswada huo na Mei, mwaka huu, serikali ya Muungano ilipeleka Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliokuwa na vifungu sita na Zanzibar waliujadili na kupeleka mapendekezo ya rasimu ya muswada huo.

“Muswada uliopelekwa Bungeni uliongezewa vifungu vingi ambavyo havikuwamo katika rasimu iliyopelekwa Zanzibar,” alisema.

Profesa Lipumba  alisema kifungu cha 26 cha sheria mama kurekebishwa kuruhusu iwapo theluthi mbili za kila upande hazitapatikana kwa mara mbili, basi kura kwa mara ya tatu itakuwa kwa wingi wa kawaida ya kila upande.

Alisema kifungu cha 37 kinachoruhusu kuvunjwa kwa Tume ya Katiba kimerekebishwa bila mashauriano katika Bunge la Katiba na siyo kama SMZ ilivyoafiki awali kuwa Tume itavunjwa baada ya matokeo ya kura ya maoni.

“Yaliyojiri Bungeni na yanayoendelea kusemwa na kutendwa na CCM na serikali juu ya muswada huo ni matokeo ya mikakati, hivyo nguvu za pamoja za wananchi, wadau na wenye kuitakia mema nchi yetu zinapaswa kuunganishwa.

MAAZIMIO YA VYAMA.

Alisema vyama hivyo vimedhamiria kuunganisha umma kufanya maamuzi ya kunusuru mchakato huo kuendelea kutekwa na kuhodhiwa na CCM kwa kuzingatia kwamba madaraka na mamlaka yote ya wananchi na serikali inapaswa kuwajibika kwa wananchi.

Aidha, alisema Septemba 21, mwaka huu, watafanya mkutano wa hadhara uwanja wa Jagwani jijini Dar es Salaam, ambao utakuwa mwanzo wa hatua za kwenda kwa wananchi ili kuwaunganisha kuchukua hatua.

Alisema mikutano hiyo itakuwa endelevu kwa maeneo mengine nchini kwa viongozi wa vyama hivyo kuzungumza na Watanzania ili kuungana pamoja kupinga mchakato kuhodhiwa.

Pia, vinawapongeza na kuwaunga mkono wabunge wa vyama vyao walioweka pembeni tofauti zao za kivyama na kutumia njia za kibunge kutaka mjadala wa muswada huo usiendelee bungeni kwa lengo la kuhakikisha masuala muhimu kwa niaba ya wananchi yanazingatiwa.

KAULI YA MBOWE

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema vyama hivyo vinaziomba asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, taasisi za elimu ya juu, vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, taasisi za sekta binafsi, watu wenye ulemavu, wataalam wa masuala mbalimbali, wanawake, vijana, vyama vya wastaafu na makundi mengine, kuweka kando tofauti zao na kujikita kwenye mchakato huo.

Aidha, alivitaka vyombo vya habari kuunga mkono na kwamba muungano huo uko tayari kushirikiana na wana-CCM na viongozi wa serikali wenye mapenzi mema na Tanzania kwa miaka 50 au 100 ijayo.

Alisema tatizo kubwa ni baadhi ya viongozi kufanya mchakato wa Katiba kama suala la kizazi cha sasa na kusahau suala hilo ni la vizazi vijavyo na Katiba ni ya Watanzania wote na si chama au viongozi.

“Mkataba wa Katiba ndiyo sehemu pekee ya Watanzania kutibu majeraha waliyonayo, CCM inapoteza mwelekeo wanatumia ubabe, kanuni na wingi wao ndani ya Bunge kuburuza mchakato wa Katiba,” alisema.

Alisema viongozi wanahubiri amani, lakini wanayotenda hayaendani na kutaka amani ya Tanzania idumu kwani licha ya kuwapo viashiria vya kutoweka kwa amani, mchakato wa Katiba unalazimishwa kuongezwa kama kiashiria kingine.

MBATIA ANENA

 

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema vyama hivyo vinamuomba Rais Jakaya Kikwete, kutosaini muswada huo kwa kuwa hautasaidia upatikanaji wa Katiba yenye ushirikishwaji wa wananchi.

“Tunamtahadharisha Rais Kikwete, historia isije ikamhukumu kwa kusaini muswada huo ambao umepitishwa kinyemela, aweke maslahi ya Taifa mbele na si chama chake ambacho ni Mwenyekiti wa Taifa…mkono wake usitumbukize Taifa kwenye machafuko,” alisema.

Aidha, vyama hivyo vimesema havitakwenda Ikulu kwa ajili ya kuonana na Rais ila zaidi vitaelekeza nguvu kwa wananchi wenye Katiba yao na kumsihi Rais kutosaini muswada huo kwa kuwa mkono wake ndiyo unasubiriwa kuamua hatma ya Taifa kwa miaka mingi ijayo.

Septemba 6, mwaka huu, wakati wa kikao cha Bunge palitokea purukushani kubwa kiasi cha wabunge na askari wa Bunge kutwangana makonde hadharani, baada ya Naibu Spika, Job Ndugai, kukataa kumruhusu Mbowe kama Kiongozi Rasmi wa Kambi ya Upinzani kutoa hoja aliyokuwa nayo.


No comments:

Post a Comment