Friday, September 13, 2013

UMOJA WA AFRIKA UNATAKA MAHAKAMA YA KIMATAIFA ICC KUSITISHA KESI ZINAZOWAHUSU VIONGOZI WA KENYA KWA SASA.

Muungano wa Afrika sasa unataka mahakama ya kimataifa ya ICC kusitisha kesi za Naibu rais wa Kenya William Ruto, Rais Uhuru Kenyatta na mwandishi Joshua Arap Sang katika mahakama hiyo hadi pale ombi lake kwa mahakama hiyo kutaka kesi hizo kurejeshwa nyumbani kuamuliwa.

AU pia inataka Bwana Ruto na Rais Kenyatta kuruhusiwa kuchagua vikao wanavyotaka kuhudhuria wakati wa kusikizwa kwa kesi zao kutokana na majukumu yao ya kikatiba.

Kwenye barua iliyoandikwa kwa ICC, AU inasema kuwa mahakama hiyo mwanzo ilipaswa kuamua ikiwa itaweza kuhamishia kesi hizo nchini Kenya kabla ya hata kuanza kuzisikiliza.

Katika barua yake kwa ICC, AU pia Imegusia swala la rufaa ambayo imewasilishwa katika mahakama hiyo na mwendesha mkuu wa mashtaka Fatou Bensouda dhidi ya kumruhusu bwana Ruto kuhudhuria tu baadhi ya vikao akisema kuwa majaji wangemlazimisha naibu rais Ruto kuhudhuria vikao vyote vya kesi yake kabla ya rufaa kuamuliwa.

Muungano huo umeelezea kuhusu mikutano mikuu miwili ya usalama inayotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu ambayo Rais Kenyatta hataweza kuhudhuria kwa sababu kesi ya naibu rais William Ruto itakuwa inasikilizwa ICC.

AU imeongeza kuwa kesi hizo zitahujumu jukumu la Kenya katika ukumbi wa kimataifa ikisisitiza kuwa hazipaswi kuathiri majukumu ya viongozi hao wawili.

AU inasema kuwa licha ya kuwa Kenya imekuwa ikiheshimu mahakama hiyo, inapaswa kufanya hivyo kwa kuzingatia Katiba yake.


No comments:

Post a Comment