Saturday, January 11, 2014

VIJANA MNAOTAKA KUWA WANASISA SOMA KITABU HIKI TUJISAHIHISHE:

Mwalimu NyerereBaba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiwa Rais wa Tanganyika African National Union, Mei 1962 aliandika kijitabu alichokipa jina la TUJISAHIHISHE. Maudhui yaliyomo kwenye kijitabu hicho yameendelea kuwa muhimu sana kwa viongozi na wananchi wa Tanzania takriban miaka 50 tangu akiandike. Endelea… 

UMOJA wa kundi lolote ni sawa sawa na umoja wa viungo mbalimbali vya mwili au mtambo. Viungo vya mwili havina budi vitii kanuni zinazoviwezesha kufanya kazi yake sawa sawa. Lakini haviwezi kutii kanuni hizo kama haviko katika hali ya afya njema. Mara kiungo kimoja kinapokuwa hakina afya safi, huanza kuvunja kanuni za kazi na mwili mzima hupata taabu.

Umoja wa binadamu na kadhalika, hauwezi kutimiza madhumuni yake bila viungo vyake kutii kanuni zinazouwezesha umoja wa binadamu kufanya kazi zake sawa sawa. Nataka kutaja makosa machache ambayo mara nyingi huzuia umoja wowote kuwa imara hata ushindwe kutimiza madhumuni yake.

Ukiondoa matatizo wayapatayo binadamu kwa sababu ya mambo kama mafuriko, nzige, kiangazi n.k, matatizo yao mengi hutokana na unafsi. Unafsi ni wa aina nyingi. Swali ambalo twalisikia mara kwa mara, hali yetu ya baadaye itakuwaje? Ni swali ambalo sina shaka kuna watu wanaouliza kwa nia safi kabisa. Lakini mara nyingi linalotokana na unafsi. Mtu anayeuliza unafikiri kuwa TANU iliundwa kwa faida yake yeye binafsi. Ni kama kwamba TANU ilipoundwa ilimwahidi kwamba ikiwa atakubali kuwa mwanachama, au kiongozi basi TANU itamfanyia yeye jambo fulani kama tunzo, anasahau kabisa kuwa TANU inajishughulisha na haja za jumuiya kwa ujumla. Lakini kwa mtu wa aina hiyo hata kama TANU inatimiza madhumuni yake ya jumuiya ataona kuwa ni umoja ambao hauna maana kwa sababu haumtimizii haja zote za nafsi yake, huu ni unafsi. Kama wanachama wa TANU, na hasa viongozi, hawatakihukumu chama chetu kwa mahitaji ya jumuiya, bali watakihukumu kwa mahitaji ya nafsi zao wenyewe, chama hakitadumu na wanachama wa aina hiyo ni ugonjwa katika chama.

Dalili nyingine ya unafsi na ambayo ni ugonjwa mbaya sana ni fitina. Kanuni moja ya TANU inasema hivi: “Nitasema kweli daima. Fitina kwangu ni mwiko.” Lakini bado tunao wanachama ambao ni wafitini wakubwa bila kujitambua. Ni wa aina mbalimbali.

Wengine humwona mwenzao anafanya kosa, badala ya kumwabia pale pale kijamaa kwamba atendalo ni kosa, watanyamaza kimya. Lakini hawanyamazi kabisa! Watakwenda kumteta katika vikundi vya siri siri. Mateto haya si ya kumsaidia mwenzao, ni ya kumdhuru. Hii ni aina mojawapo ya fitina. Wengine hugawa watu katika mafungu. “Fulani” japo akifanya kosa kubwa sana hasemwi. Lakini “fulani” wa pili akifanya kosa japo dogo, kosa lile hukuzwa likawa kama Mlima Kilimanjaro. Hawa hutafuta sababu za kumtetea “fulani” wa kwanza au za kumlaumu “fulani” wa pili ambazo hazifanani kabisa na ukweli. Kwa watu wa aina hii, ukweli ni jambo ambalo hutegemea mtu-si kitu kinachojitegemea chenyewe bila kujali mtu. “Fulani” wa kwanza akisema katika majadiliano kuwa mbili na mbili ni tano, wao watakubali. Lakini “fulani” wa pili akisema sivyo, mbili na mbili nne watamwona ni mtu mbaya kabisa ambaye hastahili hata kusikilizwa. Hawa hawajali ukweli, hujali nafsi tu. Kwao, ukweli ni maono yao na matakwa yao. Hatuna budi, hasa katika majadiliano na mazungumzo yanayohusu jumuiya, tujifunze kusikiliza hoja zenyewe zinazotolewa na wenzetu, na kuijibu zile hoja kwa kuzikubali au kuzikataa, bila kujali kama aliyezitoa ni rafiki au si rafiki. Pia wanaopingwa hawana budi wakubali kuwa kinachopingwa ni zile hoja zao, siyo wao wenyewe. Bila mazoea haya, mazungumzo hayana maana; yanakuwa ni kupoteza wakati maana huwa tumekwisha kuzihukumu hoja za mtu hata kabla hajazitamka! Kadhalika, hoja zetu zikijibiwa kwa kupingwa halafu tukawakasirikia waliozipinga tunafanya mazungumzo yasiwe na maana, kwa sababu tunapenda hoja zetu zikubaliwe tu hata kama si hoja safi.

Ukweli una tabia moja nzuri sana, haujali mkubwa wala mdogo, hujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa. Ukiniona nataka kupiga teke jiwe kwa kuwa unafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nikalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi kupuuzwapuuzwa.

Wakati mwingine mtu tunayempinga huwa ana makosa kweli, lakini hoja tunaotoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake. Nikisema mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine nafikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha. Ni kweli mbili mara tatu ni sita, lakini mbili na tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali yako kwa kusema kuwa meno yangu ni machafu, au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana. Huu ni mfano wa upuuzi, lakini mara nyingi hoja tunazotumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda, au kukubali mawazo yetu huwa hazihusiani kabisa na mambo tunayoyajadili.

Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga ni unafsi. Pengine huwa tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine twaweza kuwa hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tamaa yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana. Ni kweli kamba demokrasia haiwezi kudumu ikiwa wachache hawatakubali matakwa ya wengi. Lakini matakwa ya wengi hujulikana katika majadiliano au mazungumzo ya wazi wazi.

Kadhalika, matakwa ya wachache hujulikana katika majadiliano na mazungumzo. Bila wale wachache kusema wazi wazi matakwa yao, majadiliano hayana maana.Wakati mwingine hata baada ya majadiliano, wachache-japo wamekubali kutii uamuzi wa wengi- wanaweza kuendelea kuamini kwamba mawazo yao ni sawa, na ya walio wengi yamepotoka. Demokrasi inawapa haki na ukweli unawapa wajibu wa kuendeleza mawazo yao mpaka wengi waone kuwa ni ya kweli. Bila hivyo maendeleo katika mawazo hayawezekani, kwani mara nyingi wazo zuri hutokana na mtu mmoja tu. Mwanzo laweza likapingwa, pengine kwa nguvu kabisa, na walio wengi, lakini hatimaye wengi hulikubali. Huu ndio msingi wa maendeleo katika mawazo ya binadamu.

Makosa ni makosa na dhuluma ni dhuluma, japo watendao makosa hayo au dhuluma ile ni wakubwa au ni wengi. Chama kinachopenda ukweli na haki hakina budi kiwape wanachama wake uhuru na nafasi ya kusahihisha makosa na kuondoa dhuluma. Wanachama hawana budi waone kuwa ni wajibu wao kutumia uhuru huo na nafasi hiyo. Wanachama wasiotumia uhuru huo na nafasi kwa sababu ya kuogopa kuchukia au kupoteza nafasi zao, wanafanya kosa kubwa la unafsi, ambalo ni adui wa haki na ukweli.

Kosa jingine linalotokana na unafsi tunalifanya wakati wa kuchagua viongozi. Wakati mwingine hufanywa na wanachama; wakati mwingine hufanywa na viongozi wenyewe, au wale wanaotaka uongozi. Nimesema mahali pengine kwamba viongozi wetu hawana budi watokane na WATU. Viongozi wa TANU. hawana budi watokane na wanachama wa TANU wenyewe, bila hila,vitisho, rushwa au ujanja wa aina yoyote. Lakini mara nyingi wanachama huchagua viongozi bila kufikiri kwa makini kama viongozi hao wanaweza au hawawezi, kazi wanayochaguliwa kufanya. Wanachama wetu watafanya makosa makubwa sana ikiwa watachagua viongozi wao ovyo tu. Hii ni jambo la hatari kwa demokrasi na chama chetu, na maadui wa TANU wanaweza kusema kwamba demokrasi haina maana kwa sababu haizai viongozi wanaoweza kazi zao! Hii si kweli, maana wote twajua kwamba demokrasi inaweza kuchagua viongozi wazuri. Lakini ni wajibu wetu katika kuhifadhi demokrasi kuona kuwa inachagua viongozi ambao wanaziweza kazi zao. Kazi ya kuchagua viongozi ni kazi ya wanachama wetu; kwamba jambo hili ni kubwa sana. Haifai kuchagua kiongozi kwa sababu ni mjomba, au binamu au ana sauti au sura nzuri. Wala haifai kuacha kumchagua mtu kuwa kiongozi kwa sababu kama hizo. Jambo kubwa ni kuchagua kiongozi mwenye tabia nzuri na anayeweza kazi. Hatuna budi tutii kanuni hii katika kuajiri wafanya kazi katika TANU au serikalini. Hawa pia hawana budi wachaguliwe kwa sababu wanaiweza kazi wanayoajiriwa kufanya, na ni watu wenye tabia nzuri.

Kosa jingine ni kutojielimisha. Kanuni yetu moja inasema: “Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu wote na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote.” Wengi wetu hufikiri kuwa kujielimisha ni kwenda Kivukoni, au kupata nafasi kwenda kusoma katika nchi za nje. Wengine hufikiri kuwa kujielimisha ni kujua kusoma na kuandika. Hilo ni kosa, lakini si kubwa kama la pili, wengi wetu hasa baadhi ya viongozi hufikirikuwa tunajua kila kitu na hatuna haja kujifunza jambo lolote zaidi. Mtaalamu mmoja wa zamani alisema kuwa mwanzo wa elimu ni kutambua kuwa hatujui kitu.

Nimesema kwamba wengine wetu wanafikiri kuwa kujielimisha Kivukoni au kupata nafasi kwenda kusoma nchi za nje, kwa kweli moja ya taabu zetu kubwa ni kwamba watu wengi sana wangependa wapate nafasi ya kwenda kusoma katika nchi za nje, na chama kinashindwa kuwaridhisha wote. Tamaa ya kupata elimu ni tamaa nzuri sana; ndiyo maana kupata elimu ni moja ya kanuni zetu tisa. Lakini kudai kwenda kupata elimu nje ya Tanganyika au pahali fulani, na halafu kunug’unika matakwa yetu yasiporidhishwa, ni jambo lisilokuwa na msingi. Tunajua kwamba elimu ni jambo la lazima kwa kila raia, lakini tunajua kwamba pia kila raia hawezi kupata nafasi ya kwenda nje ya Tanganyika kupata elimu; au kuingia pahali fulani kupata elimu. Jambo la maana ni kujua ziko nafasi ngapi nje ya Tanganyika au ndani ya Tanganyika na kama TANU na serikali huzijaza nafasi hizo kwa njia ya haki.

Kujielimisha siyo maana yake kwenda shuleni. Kama hivyo ingekuwa ndivyo, TANU ingekuwa imefanya kosa kubwa sana kumtaka kila mwanachama ajitahidi kujielimisha na kutumia elimu yake kwa ajili ya wote. Kujielimisha ni kutafuta ukweli wa mambo. Kwenda shule hutusaidia. Lakini japo hatuwezi kwenda shule twaweza kujifunza. Kijiji chetu hakina maji ya kutosha. Kujielimisha ni kujua kwa nini kijiji chetu hakina maji ya kutosha; na baada ya kujua sababu yake, lazima tujielimishe zaidi kwa kutafuta njia zinazoweza kukipatia kijiji chetu maji ya kutosha. Au kijiji kina ugomvi daima.Kujielimisha ni kutafuta sababu za kweli zinazofanya kijiji chetu kiwe na ugomvi daima na badala ya hapo kutafuta njia za kuondoa ugomvi katika kijiji chetu. Elimu ya kweli ni ujuzi wa sababu za mambo mbalimbali; na kama ni mambo mabaya ni kujua jinsi ya kuyaondoa; na kama ni mema, jinsi ya kuyadumisha. -------- ni yule anayeyapa mambo sababu zisizo za kweli na kushauri dawa isiyo ya kweli katika kutafuta sababu za matatizo, na jinsi ya kuyaondoa. Kila mmoja wetu anacho chombo cha kutumia-akili yake. Jambo la maana ni kuzipa akili uhuru kamili wa kutafuta elimu bila kutiwa kiinimacho na utashi wetu wa unafsi.

Watu waliohatari sana ni wale ambao wanafikiri kuwa wanajua kila kitu, wala hawana haja kujifunza zaidi. Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia kabisa maendeleo. Sababu moja ambayo ilituzuia sisi Waafrika kuendelea ni majibu ya urahisi kwa matatizo makubwa. Shamba letu kama halikutoa mavuno ya kutosha, jibu lilikuwa wazi; au limelogwa au ni amri ya Mungu. Watoto wetu walipokuwa wagonjwa daima, jibu lilikuwa rahisi; au walilogwa au ni amri ya Mungu. Nyumba yetu ilipopigwa radi ikaanguka, jibu lilikuwa rahisi; au ni uchawi au ni amri ya Mungu. Majibu ya namna hii huzuia binadamu kupata sababu za kweli za matatizo yao, na kwa hiyo yanazuia akili kutafuta njia za kweli za kuondoa matatizo hayo.

Siku hizi, tumeanza kutumia majibu mengine rahisi, mambo yakienda mrama, badala ya kutumia akili zetu na kutafuta sababu za kweli, tunalamu Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n.k. Yawezekana kweli kwamba kosa ni la Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n. k.-lakini yafaa akili ifikie jibu hilo baada ya uchaguzi wa kweli, siyo sababu ya uvivu wa kutumia akili! Uvivu wa kutumia akili unaweza kufanya tutumie dawa kuondoa matatizo ambayo si dawa hata kidogo. Nikienda kwa mganga anitibu maradhi yangu, namtazamia kuwa kazi yake ya kwanza ni kujua hasa, siyo kwa kubahatisha, naumwa nini; kazi yake ya pili ni kujua sababu ya ugonjwa wangu; kazi yake ya tatu ni kujua dawa ya ugonjwa wangu. Daktari asipojua ugonjwa wangu na sababu zake hawezi kujua dawa yake. Akinipa dawa nikapona, atakuwa kaniponya kwa bahati tu, kwa desturi daktari wa namna hiyo hawezi kumponya mgonjwa, na ni daktari wa hatari sana.

Kadhalika, chama ambacho nia yake ni kuwa daktari wa matatizo ya jumuiya hakina budi kiwe na tabia ya kujua matatizo yenyewe, sababu za matatizo hayo, na dawa yake. Bila kujua matatizo na sababu za matatizo hayo hakiwezi kujua dawa yake. Daktari anayejidai kuwa anajua kila kitu, na kumbe hajui kitu, ni hatari zaidi kuliko daktari anayekiri kuwa hajui kitu. Kadhalika, kiongozi anayejidai kuwa anajua kila kitu, na kumbe hajui, ni hatari zaidi kuliko yule anayekiri kuwa hajui kitu na yuko tayari kujifunza. Kwa kweli huyu wa pili si hatari hata kidogo kwa sababu kama nilivyosema mapema, ufunguo wa elimu ni kule kutambua kuwa hatujui kitu!

Kosa jingine, na hili husumbua na kubabaisha sana wenzetu, ni kufanya mawazo na matakwa ya nafsi zetu kuwa ni mawazo na matakwa ya raia. Nimesema mbeleni kwamba hatuna budi tuone daima kwamba mambo tunayoyazungumza yanatokana na watu, au mawazo yetu yanakubaliwa na watu. Mara nyingi jambo hili halitokei. Kuna wenzetu ambao wakileta madai ambayo wanajua yatakataliwa na wenzao kwa sababu hayana maana, basi huyahimili kwa kwa kusema kuwa ni ya wananchi. Mara ngapi tumesikia viongozi fulani wakisema: “Wananchi wote wa upande ninaotoka wanataka jambo hili?” Viongozi hawa huwa mara nyingi hawakuzungumza jambo hilo na mwananchi yeyote. Lakini hawaoni haya kuja kubabaisha wenzao kwa kusema kuwa ni jambo linalotakiwa au lisilotakiwa na wananchi wote! Tabia hii ni mbaya kwa sababu inaondoa ukweli katika mazungumzo. Njia fupi ya kujaribu kuonyesha kwamba mtu asiyekubaliana na kiongozi huyo, basi anapinga mawazo au matakwa ya wananchi wote.

Kosa jingine kubwa ni kuwagawa watu katika makundi; kundi “letu” na kundi “lao”. Wakati mwingine “sisi” ni viongozi tunaochaguliwa kwa kura za wanachama. Hili ndilo kundi letu. Viongozi wengine ni wale wanaoajiriwa. Baadhi ya viongozi wanaochaguliwa hujiona kuwa ni mabwana na kwamba viongozi wanaoajiriwa ni watumishi tu ambao hawastahili kuheshimiwa. Lakini mara nyingi viongozi wengi wanaoajiriwa huwa wanawazidi wengi wa wale wanaochaguliwa katika mambo ya elimu. Basi, wao pia huunda “ubwana” wa elimu na kupuuza viongozi waliochaguliwa. Kosa hili kwa pande zote mbili ni baya. Linagawa viongozi katika makundi, na ni wazi kwamba viongozi wakigawanyika katika makundi chama pia huwa kimo katika hatari ya kugawanyika katika makundi na kukosa shabaha yake.

Lakini pengine huwa kundi “letu” ni kubwa zaidi. Kwa mfano, japo baadhi ya madhumuni ya chama chetu ni kumpatia elimu kila mtu, baadhi ya wanachama wetu huwa na mashaka na watu wenye elimu-siyo kwa sababu ya makosa yanayojulikana, lakini kwa sababu ya elimu. Tabia hii inaleta mazoea ya kusema na kukashifu elimu na ujuzi kama kwamba ni dhambi. Na hasa kwa sababu wakoloni zamani walikuwa wakituambia kuwa hatuwezi hili wala hatuwezi lile kwa sababu hatuna elimu na ujuzi wa kutosha, basi leo, kiongozi akisema kwamba kazi fulani inahitaji elimu na ujuzi wa kutosha, huonekana kuwa ana mawazo ya kikoloni! Lakini ni dhahiri kwamba chama cho chote ambacho kimetajwa “ujinga”yaani ukosefu wa elimu au ujuzi- kuwa ni baadhi ya maadui wake, hakina budi kiheshimu elimu na kiitumie. Ni dhahiri kwamba yule asiyetambua ubora wa elimu na ujuzi ni mjinga ambaye chama hakina budi kimsaidie kwa kumwondolea adui huyo anayemsumbua, yaani ujinga! Mtu yeyote akikosa na tumlaumu kwa makosa yake, lakini tusimtilie mashaka bure kwa sababu ya elimu, kwani kuwa na elimu si kosa.

Mara nyingi wenye elimu hufanya kosa hili hili la kuwatilia mashaka au kuwadharau wale wasio na elimu. Mara ngapi tumesikia watu wakikashifu halmashuri fulani siyo kwa kosa lolote ambalo limefanywa na halmashauri hiyo, lakini kwa sababu halmashauri yenyewe ni ya watu ambao hawana elimu? Hii ni kosa linaloudhi zaidi. Mtu ambaye kapewa nafasi ya kuweza kuona anapofanya mambo kama kipofu hukatisha tamaa zaidi kuliko kama angekuwa ni kipofu kweli.

Pengine kundi “letu” ni la Waafrika kwa ujumla, na kundi “lao” ni la wasio Waafrika kwa ujumla. Hasa katika nchi kama yetu mgawanyo huu unayo hatari ya kuzuia akili ya baadhi ya ndugu zetu kufanya kazi kabisa. Kwa ndugu zetu kama hao asiye wa kundi “letu” hawezi kusema lolote lenye maana. Lolote atakalolisema au kutenda huwa ni baya. Baadhi yetu hata wameanza kusema kuwa sisi Waafrika ni watu bora kuliko watu wa mataifa mengine. Huu ni ugonjwa ule ule nilioutaja mapema unaomfanya mtu kuzihukumu hoja za mwenzake kuwa ni nzuri au mbaya kabla hata hajazisikia.

Pengine kundi “letu” ni sisi wanaTANU, na “lao” ni la wale wasiokuwa wanaTANU. Kwa mfano, baadhi ya wanaTANU husahau kabisa kuwa baadhi ya watumishi wa serikali ni wananchi safi kabisa kama sisi, na pengine kuwazidi wengine wetu. Lakini kwa sababu hawana kadi za TANU, basi hufanywa kuwa si kitu. Pengine huongezeka kosa lile lile la kuwafanya wao kuwa ni watumishi tu ambao hawastahili heshima yoyote ya utu. Pengine kwa sababu baadhi yao wanayo elimu nzuri, huongezeka kosa lile lile la kuwatilia mashaka wenye elimu. Sisemi kwamba huwa hawana budi wahukumiwe kwa makosa yao ya kweli, si kwa kubwagwa tu katika kundi la walaumiwa bila makosa yao wenyewe.

Mungu ametupa akili ili tuweze kuzitumia kwa manufaa yetu na ya jumuiya. Makosa niliyoyataja, na mengine mengi ambayo kila mtu aweza kuyafikiria mwenyewe, huzinyima akili uhuru wa kufanya kazi yake barabara. Huwa kama ni kitu kinachokizuia chombo kufanya kazi yake vizuri. Ni wajibu wetu kujitahidi kadiri iwezekanavyo kuzipa akili zetu uhuru wa kufanya kazi bila kutu na uchafu wa aina nilioutaja.

Yawezekana kuwa mara nyingi makosa tanayofanya sisi hutokana na makosa ya wengine. Kumtia mashaka mtu anayekutilia mashaka ni jambo la kibinadamu. Kumrudishia kofi mtu aliyekupiga kofi ni jambo la kibinadamu siyo kusema kuwa ni kitendo cha busara. Kipofu akinivamia na kuniumiza, nikikasirika kwa sababu ya maumivu aliyonitia ni jambo la kibinadamu, lakini nikijitoboa macho ili na mimi nimvamie na kumwumiza haitakuwa nimefanya jambo la busara.

Nimejaribu kueleza makosa machache ambayo yafaa tuyaondoe na kuyaepuka katika chama chetu. Sitaki mtu yeyote afikiri kuwa mimi niliyeandika maneno hayo sinayo makosa hayo. Hivyo si kweli. Kosa moja kubwa sana ambalo linatokana na unafsi ni kutaja makosa ambayo sisi wenyewe hatunayo, na kuficha makosa ambayo sisi wenyewe tunayo. Hii ni kosa lile lile linalotufanya tulaumu tusiowapenda, na kutolaumu tunaowapenda, bila kujali ukweli. Nimetaja makosa haya ili yatusaidie, siyo katika kuwahukumu wenzetu tu ambalo ni jambo rahisi, lakini katika kujihukumu sisi wenyewe, ambalo ni jambo gumu na la maana zaidi.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment