Thursday, March 27, 2014

"KUNA NJAMA ZA KUVURUGA BUNGE LA KATIBA" - SITTA

Baada ya jana jioni kuahirisha Bunge hilo baada ya kutokea sitofahamu ya kubadilisha kanuni, Sitta alikutana na waandishi wa habari na kusema kwamba kuna njama za baadhi ya wanasiasa kutumia vurugu kuhujumu mchakato wa upatikanaji wa Katiba, badala ya kujenga hoja.

Bila kuwataja wanasiasa hao, Sitta alisema ikiwa hawataki kuendelea na mchakato huo, basi waondoke na kuwaacha wenye nia njema.

“Wanasiasa hawa wamedhamiria kuvuruga mchakato wa Katiba, tuhuma ambazo tumetuhumiwa leo na Lissu (Tundu) ni uongo na uzushi, mimi sihusiki na kupeleka marekebisho ya kanuni kwenye Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge,” alisema Sitta.

Sitta alikuwa anajibu mchango wa mjumbe wa Bunge, Tundu Lissu alioutoa mapema kwenye kikao cha jioni, akipinga kilichoelezwa ni njama za kutaka kubadili kanuni kinyemela ili kumsaidia mwenyekiti kulidhibiti Bunge.

Sitta alisema kwa kuzingatia kanuni ya 59 (1), Kamati ya Uongozi ina mamlaka ya kupeleka marekebisho ya kanuni ili kuliwezesha Bunge kufanya kazi vizuri.

Alisema hoja kwamba haiwezekani kufanyika mabadiliko hata kabla ya kuanza kutumika kanuni, siyo ya msingi kwani kila kitu kinabadilika kutokana na mazingira yake.

“Kamati ya Uongozi ndiyo ilipeleka waraka wa mabadiliko ya kanuni kwa Kamati ya Kanuni na Haki kwa kuzingatia kanuni, lakini hata kabla ya kujadiliwa na kamati husika inaonekana kuna wajumbe ndiyo wameichukua na kuifikisha bungeni,” alisema Sitta.

Alisema kwa kiasi kikubwa marekebisho ambayo yangesomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, yalilenga kutoa ufumbuzi wa kanuni ya 37 na 38 juu ya upigaji kura ama uwe wa wazi au siri.

Sitta alisema pamoja na hilo, kulikuwa na marekebisho ya msingi kama kuweka utaratibu mzuri wa majadiliano katika kamati pia kuweka utaratibu wa vikao vya Bunge kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.

“Mengi ambayo alikuwa anayasema Lissu kama ni takataka hayakuwapo katika taarifa ya Kificho,” alisema Sitta.


No comments:

Post a Comment