Kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC) na Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), katika Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu.
Jopo la majaji hao litaongozwa na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu ambaye atasaidiana na Dk. Fauz Twaib na Augustine Mwarija.
Katika kesi hiyo ambayo ilifunguliwa Agosti Mosi, mwaka huu,
wanaharakati wameiomba mahakama hiyo itoe tafsiri za kisheria katika
baadhi ya Ibara ndani ya Katiba, zinazokinzana.
Hata hivyo, kesi hiyo namba 24/2013 bado haijapangiwa tarehe ya kuanza
kusikilizwa, ambayo hati ya mashtaka inaonyesha kwamba washtakiwa ni
Waziri Mkuu, Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick
Werema.
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa na mawakili wasiopungua
20 akiwamo Haroud Sungusia wa LHRC na Francis Stolla ambaye ni Rais wa
TLS.
Walalamikaji katika hati ya madai wamewasilisha maombi mawili; moja
wakiitaka mahakama itoe tafsiri ya kisheria katika Ibara mbili za Katiba
ile ya 100 (1) na 13 (2).
Wakiongozwa na Wakili Sungusia wanaomba ufafanuzi wa kisheria katika
ibara ya 100 (1) ya Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa majadiliano
bungeni.
Ibara hiyo inaeleza kwamba: “Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na
utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo
chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika mahakama au mahali
penginepo nje ya bunge.”
Hati hiyo inafafanua zaidi kwamba Ibara hiyo ina ubaguzi ndani yake
kwani inatoa uhuru wa majadiliano bungeni hata kama mbunge atavunja haki
za mtu mwingine hataweza kushitakiwa wala kuhojiwa jambo ambalo
linakinzana na Ibara ya 13 (2) ya Katiba.
Ibara hiyo inaeleza kwamba: “Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa
na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo
ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.”
“Tunaomba mahakama hiyo itamke wazi kuwa Ibara ya 100 (1) inakwenda
kinyume cha matakwa ya Ibara 13(2), zinakinzana kwani Ibara hiyo ya 100
(1) ya Katiba inatoa haki tu kwa upande mmoja wa wabunge uhuru wao
kutohojiwa na inawanyima haki ya kuwahoji au kuwashitaki wabunge
wanaotoa kauli zao bungeni hata kama kauli hizo za wabunge zimevunja
haki za wananchi, hivyo tunaomba mahakama itamke kuwa ibara ya 100 (1)
ya Katiba inakinazana na ibara hiyo.”
Ombi la pili katika hati hiyo ni kuiomba mahakama hiyo itamke kuwa kauli
ya Pinda ambayo ililitaka Jeshi la Polisi kuwapiga wale wote wanaokiuka
amri za jeshi hilo, kama kauli hiyo nayo inalindwa na kinga iliyowekwa
katika Ibara ya Ibara ya 100 (2) ya Katiba ya nchi ambayo inatoa kinga
ya majadiliano ndani ya Bunge.
Ibara hiyo inaeleza kwamba: “Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya
sheria nyingine yoyote inayohusika, mbunge yeyote hatashtakiwa au
kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote
alilolisema au kulifanya ndani ya bunge au alilolileta bungeni kwa njia
ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo.”
Katika kauli hiyo, Pinda alisema: “Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua wewe kukaidi utapigwa tu.
Maana hakuna namna nyingine; lazima tukubaliane kuwa nchi hii
tunaiendesha kwa misingi ya kisheria, sasa kama umekaidi hutaki, unaona
kama wewe ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi watakupiga tu na mimi
nasema muwapige tuu kwa sababu hakuna namna nyingine, maana tumechoka
sasa,” alisema Waziri Mkuu.
Wakili Sungusia alisema wameiomba mahakama iamue kipi kinabaki kati ya haki za binadamu na kinga ya Bunge.
|
No comments:
Post a Comment